Na mwandishi wetu
Kocha Mkuu wa Coastal Union, Mwinyi Zahera amemtaka kiungo mshambuliaji mpya wa timu hiyo, Ibrahim Ajibu (pichani) kuitumia nafasi aliyompa kwa uzito wa juu vinginevyo akishindwa hapo atakuwa amepotea kabisa kwenye soka.
Ajibu ni miongoni mwa sura mpya zinazounda kikosi cha Coastal Union kuelekea msimu ujao wa Ligi Kuu NBC na michuano ya Kombe la Azam (ASFC).
Zahera ameeleza kuwa yeye ni kati ya makocha wanaotambua uwezo na kipaji alichonacho Ajibu ndio sababu akaamua kumsajili kwenye timu hiyo akiamini atambadilisha na kurudi kwenye kiwango chake kama ilivyokuwa awali.
“Ajibu ni miongoni mwa wachezaji wachache wenye kipaji kikubwa cha kucheza mpira, nilifanya naye kazi pale Yanga, nikampa hadi unahodha anachotakiwa kufanya ni kucheza kwa kujitoa kuipigania timu yake, hii ni nafasi yake ya mwisho kwenye soka,” alisema Zahera.
Kocha huyo mwenye uraia wa nchi mbili za DRC Congo na Ufaransa alisema hata hapo Coastal ameamua kumpa unahodha anachoamini atamfua yeye pamoja na wachezaji wengine ili kumrudisha kwenye ubora wake.
Tangu atoke Yanga misimu mitatu iliyopita Ajibu amezichezea timu tatu tofauti ambazo ni Simba, Azam FC na Singida Fountain Gate na kote huko hakuonekana na mchango kwenye timu kiasi cha kutolewa kwa mkopo au kuvunjiwa mkataba.
