Sydney, Australia
Baada ya timu ya wanawake ya Nigeria au Super Falcons kutolewa kwenye fainali za Kombe la Dunia, imebainika kuwa wachezaji wa timu hiyo wanadai posho na marupurupu ya tangu mwaka 2021.
Nigeria imetolewa na England kwa mikwaju ya penalti 4-2 lakini habari nyingine mbaya ni kwamba wachezaji wa timu hiyo kwa sasa wanasaidiwa na Umoja wa Wachezaji Duniani (FifPro) kudai stahiki zao za tangu mwaka juzi.
Taarifa ya FifPro imethibisha kuhusu madai hayo na namna wachezaji hao wanavyosumbuliwa katika kufuatilia suala hilo kwa uongozi wa Shirikisho la Soka Nigeria (NFF) kabla na hata wakati huu fainali hizo zikiendelea.
Kwa mujibu wa FifPro wachezaji wa Super Falcon wamejizuia kwa muda mrefu kutoa taarifa hizo hadharani katika kipindi hiki cha fainali za Kombe la Dunia lakini wanaamini huu ni wakati sahihi kwa viongozi wa NFF kutekeleza wajibu wao kwa kulipa madeni hayo.
“Nimeona mahitaji ya msingi waliyonayo England, Nigeria hatuna, viwanja vyetu vya mazoezi si vizuri, mahali tulipokuwa tunalala si pazuri, kuna wakati tulikuwa tunalala wawili kitanda kimoja,” alisema mshambuliaji wa timu hiyo, Ifeoma Onumonu.
“Kuna mengi yanatakiwa kufanywa, ni matumaini yangu kwamba watu wengi wataanza kulizungumzia hili, ni vigumu kufanya vizuri, tumefanya tulichoweza kufanya kwa sababu tunapenda kuichezea nchi yetu lakini wanachukulia rahisi suala la sisi kucheza katika ubora,” alisema Ifeoma.
Nigeria licha ya kuwa miongoni mwa mataifa makubwa ya Afrika lakini imekuwa na matatizo ya mara kwa mara na timu hiyo, mwaka 2019 na 2022 wachezaji walikwama katika hoteli kwa kilichodaiwa kuwa ni NFF kuwa na madeni katika hoteli hizo.
Habari za ndani zinadai kwamba mara baada ya wachezaji wa timu hiyo kuwasili Australia kwa ajili ya fainali hizo walishtushwa na taarifa za kwamba malipo yao ya dola 30,000 kwa kila mchezaji yalizuiwa
Kocha wa timu hiyo, Randy Waldrum naye aliingia katika mzozo na NFF baada ya taarifa yake kwenye mitandao ya kijamii akiwashutumu viongozi wa shirikisho hilo kwa usimamizi mbovu wa timu huku akidai kwamba hata yeye hajalipwa baadhi ya fedha zake.
Baada ya Waldrum kutoa kauli hiyo, mkurugenzi wa mawasiliano wa NFF, Ademola Olajire alinukuliwa akisema kwamba kocha huyo raia wa Marekani ni msema ovyo na ni kocha wa hovyo katika historia ya makocha waliowahi kuinoa Super Falcons.
Nigeria ilifuzu hatua ya mtoano katika fainali hizo ikitokea Kundi B ambapo ilitoka sare mbili dhidi ya Canada na Jamhuri ya Ireland pamoja na ushindi wa mabao 3-2 dhidi ya wenyeji Australia.
Kombe la Dunia Wachezaji Nigeria wadai posho za mwaka juzi
Wachezaji Nigeria wadai posho za mwaka juzi
Related posts
Read also
