Na mwandishi wetu
Nyota wa Dallas FC ya Marekani, Bernard Kamungo amesema yuko tayari kuitumikia timu ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars huku akionesha furaha yake kwa kuifunga timu ya Inter Miami, ambayo Lionel Messi ni nahodha wake.
Winga huyo alisema hayo baada ya kugeuka gumzo kufuatia bao alilofunga na kiwango alichoonesha usiku wa kuamkia jana katika mechi ya hatua ya 16 bora ya Kombe la Ligi dhidi ya Inter Miami.
Kamungo (pchani juu akiwa na Messi) aliyefunga bao la pili na kuipa Dallas uongozi wa mabao 2-1 hadi mapumziko.
Kamungo pia alielezea furaha yake kwa kufunga mbele ya Messi, nahodha wa Argentina ambaye naye alifunga mabao mawili katika sare ya mabao 4-4 ya dakika 90 za awali kabla ya Dallas kutolewa kwa matuta 5-3.
“Yaani sijui hata niseme vipi kwa sababu pia sikuwahi kufunga bao mbele ya Imani (kaka yake aliyekuwa uwanjani, Uwanja wa Toyota), ilikuwa mara ya kwanza kufunga mbele yake na ilikuwa nimefunga dhidi ya Messi, ni kitu kikubwa,” alisema.
“Timu ya taifa niliitwa mara ya mwisho (dhidi ya Niger) lakini moja ya sababu ya kutoonekana na wengi wanajiuliza ilikuwaje, ilikuwa ni masuala ya pasi ya kusafiria, pasi ilichelewa kidogo ndio maana ikashindikana ila naamini kama kila kitu kitakwenda sawa, mwezi ujao mechi ya Algeria nitakuwepo, ikitegemea na taifa litakavyoamua lakini mimi niko tayari kuitumikia Tanzania,” alisema Kamungo.
Kamungo, 21 anayetajwa kutoka kambi ya wakimbizi Kigoma kabla ya kutimkia Marekani mwaka 2017, alianza soka lake la kulipwa katika klabu ya North Texas inayoshiriki Ligi Daraja la Tatu Marekani kabla ya kujiunga na Dallas Agosti mwaka jana kwa mkataba wa miaka mitatu.
