Sydney, Australia
Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa) linachunguza tuhuma zinazomkabili kocha wa timu ya wanawake ya Zambia, Bruce Mwape (pichani) anayedaiwa kumpapasa kifuani mchezaji wa timu hiyo bila ridhaa yake.
Taarifa ya Fifa ilithibitisha kupokea tuhuma hizo ambapo Mwape anadaiwa kumfanyia kitendo hicho mchezaji wake Julai 29 wakati timu ya taifa ya Zambia ikiwa mazoezini nchini New Zealand.
Wakati Fifa ikieleza kupokea tuhuma hizo na kuzifanyia kazi, Chama cha Soka Zambia (FAZ) kimedai kutopokea malalamiko yoyote dhidi ya kocha huyo aliyeiwezesha Zambia kufuzu fainali za Kombe la Dunia zinazoendelea nchini New Zealand na Australia.
Mwape anadaiwa kufanya kosa hilo wakati wa mazoezi siku mbili kabla ya mechi ya mwisho ya Zambia ya hatua ya makundi dhidi ya Costa Rica, mechi ambayo Zambia ilishinda kwa mabao 3-1 ikiwa ni ushindi wa kwanza wa timu hiyo kwenye fainali hizo.
Taarifa ya msemaji wa Fifa ilieleza kuwa shirikisho hilo linachukulia kwa nguvu zote tuhuma za ukosefu wa maadili na imeweka wazi taratibu za kufuatwa kwa mtu yeyote katika soka ambaye anataka kuripoti tuhuma hizo.
Katika hatua nyingine, taarifa ya FAZ hata hivyo ilieleza kwamba mazoezi yote ya timu hiyo ambayo tayari imerejea nyumbani, yalirekodiwa na hakuna picha zinazoonesha tukio lolote baya.
FAZ pia walifafanua kwamba timu ya waandishi wa Fifa walikuwa wakirekodi mazoezi ya timu hiyo maarufu Copper Queens.
Kocha Mwape ambaye alikabidhiwa jukumu la kuinoa timu hiyo mwaka 2018, hii si mara ya kwanza kujikuta katika kashfa hiyo, mwaka jana mitandao ya kijamii ilimtaja ikimhusisha na kashfa za kuwafanyia wachezaji wake vitendo vya udhalilishaji kijinsia.
Mara baada ya kuibuka kwa tuhuma hizo FAZ walidai kutopokea rasmi tuhuma zozote dhidi ya Mwape ingawa iliahidi kufanya uchunguzi kama kutakuwa na ushahidi.
Kabla ya Zambia kutolewa kwenye fainali za Kombe la Dunia, Mwape aliulizwa kuhusu tuhuma hizo lakini alikana na aliwahi kuvunja mkutano na waandishi wa habari kwa sababu ya kuulizwa swali hilo zaidi ya mara moja.
Mmoja wa wachezaji wa Copper Queens alinukuliwa akidai kwamba Mwape akimhitaji mchezaji wake kimapenzi, mchezaji huyo hana haki ya kusema hapana.
Kimataifa Kocha Zambia adaiwa kumpapasa mchezaji kifuani
Kocha Zambia adaiwa kumpapasa mchezaji kifuani
Read also
