Las Vegas, Marekani
Beki wa kati wa Man United, Lisandro Martínez (pichani) amewataka wachezaji wanzake kuendelea kufokeana baada ya Andre Onana kumfokea Harry Maguire katika mechi dhidi ya Borussia Dortmund.
Onana alimfuata Maguire na kumfokea baada ya beki huyo kutoa pasi kwa kiungo Christian Eriksen, pasi iliyoonekana kuwa dhaifu katika mechi ambayo Man United ililala kwa mabao 3-2.
Wakati mshambuliaji wa zamani wa Aston Villa, Gabriel Agbonlahor akidai kukerwa na alichofanya Onana kwa Maguire, Martinez amewataka wachezaji wenzake kufokeana mara kwa mara katika msimu huu.
“Ni jambo zuri kwa timu…, ni jambo zuri, ukiwa makini zaidi utagombana hata na wachezaji wenzako, utahitaji kuhakikisha kila mmoja wenu anakuwa ‘sharp’, lakini hakuna kubwa katika hilo bali ni sehemu ya soka,” alisema Martínez.
Martínez anamjua vizuri Onana tangu wakiwa pamoja Ajax. Onana ambaye ni raia wa Cameroon, ametua Man United akitokea Inter Milan kuchukua nafasi ya David de Gea ambaye ameihama timu hiyo akiwa mchezaji huru.
“Ana msimamo, anaweza kucheza soka anajua kukabiliana na presha, yuko makini, ni kiongozi na hiyo ndiyo staili ya Manchester United,” alisema Martinez.
Martínez anayesifika kwa kucheza kibabe ambaye pia ni mchezaji wa timu ya Taifa ya Argentina, amerudi kwa mara nyingine kwenye kikosi cha kwanza cha Man United baada ya kusumbuliwa na majeraha ya mguu.
