Na mwandishi wetu
Uongozi wa klabu ya Simba hauna pingamizi kuhusu kurejea kwa mkopo kwa mshambuliaji wao wa zamani Luis Miquissone anayekipiga Al Ahly ya Misri iwapo kocha Pablo Franco atakubaliana na hilo.
Imeelezwa kuwa mchezaji huyo tangu atue Al Ahly mwanzoni mwa msimu huu hana furaha kutokana nakukosa nafasi kikosi cha kwanza na amekuwa akitajwa kutaka kurejea Simba kabla ya hivi karibuni kuibuka taarifa kwamba Al Ahly imependekeza kumrejesha Miquissone Simba kwa mkopo.
Taarifa zaidi kutoka duru mbalimbali za Misri zinaeleza kuwa timu hiyo inajipanga kuimarisha kikosi chake kuelekea msimu ujao ikitaka si tu kutwaa taji la Klabu Bingwa Afrika bali kutwaa ubingwa wa klabu wa dunia, hivyo miongoni mwa majina ya watakaopunguzwa la Miquissone lipo pia.
Mwenyekiti wa Simba, Murtaza Mangungu amefafanua kuwa wao hawana pingamizi la kurejea kwa Miquissone kwa kuwa wao si tatizo mchezaji mzuri anapoamua kurudi alipotoka na kwamba wao hawatakuwa wa kwanza kufanya hivyo.
“Miquissone ni kijana wetu na hawa wachezaji mara nyingi wanapotoka kwenda timu nyingine huwa wanategemea mambo kuongezeka zaidi lakini kama inakuwa tofauti tunaweza kumpokea na hatutakuwa wa kwanza kufanya hivyo.
“Kuhusu kama kuna mawasiliano baina yetu na Al Ahly kuhusu dili hilo siwezi kusema ndiyo au hapana lakini hizi timu huwa tunawasiliana kila wakati na kama kuna jambo kama hilo nadhani wakati muafaka wa kulizungumzia ni mwisho wa msimu na si sasa tukiwa katikati ya msimu.
“Na hiyo ikiwa baada ya kusikiliza maoni ya kocha yeye anaonaje kuelekea msimu ujao na anatakaje, kwa hiyo atatutambia ilivyo na sisi tutaona itakavyokuwa lakini kwa sasa bado,” alisema Mangungu.
Hivi karibuni Simba ilimrejesha kiungo wake, Clatous Chama akitokea RS Berkane ya Morocco alikodumu kwa nusu msimu hivyo huenda ikafanya uamuzi wa kumrejesha Miquissone pia ili irejee kwenye makali yake ya awali.
Soka Hatma ya Miquissone Simba mikononi mwa Pablo
Hatma ya Miquissone Simba mikononi mwa Pablo
Read also
