Na mwandishi wetu, Mwanza
Bondia Karim Mandonga maarufu Mtu Kazi, ‘ameshindwa kazi’ usiku wa Jumamosi hii baada ya kulambishwa sakafu kwa ngumi moja kali ya bondia wa Uganda, Golola Moses.
Katika pambano hilo lililofanyika kwenye Ukumbi wa Malaika mjini hapa, mabondia hao wanaosifika kwa majigambo, waliianza raundi ya kwanza kwa kila mmoja wao kujiamini na kurushiana ngumi za hapa na pale.
Raundi ya pili, Mandonga alianza kuonesha uhai huku akishangiliwa na mashabiki wake waliojaa matumaini kwamba bondia wao angetoka ulingoni na ushindi japo mabondia hao kuna wakati walikuwa wakikumbatiana na mwamuzi kuingilia kati.
Katika raundi ya tatu, matumaini ya mashabiki wa Mandonga yalizidi kuwa juu hasa alipokwepa ngumi kali ya mkono wa kushoto ya Golola huku akijibu mapigo kwa Golola ambaye alionekana kama ameanza kuchoka.
Hata hivyo mambo yalibadilika katika raundi hiyo mabondia hao walipoanza kukumbatiana na baada ya kuachana Mandonga alirusha ngumi ya mkono wa kushoto na hapo hapo Golola akamsukumizia ngumi ya mkono wa kulia iliyompata upande wa kushoto karibu na sikio na kuanguka chini.
Kwa namna alivyoanguka, Mandonga alionesha dalili za kutoendelea na pambano na hapo hapo mwamuzi akamaliza mchezo na Golola kutangazwa mshindi japo Mandonga alionekana kama kushangaa asiamini uamuzi uliofikiwa.
Kama ilivyo kwa Mandonga, Golola naye anasifika kwao Uganda kwa majigambo kabla ya mapambano yake na amezoeleka zaidi nchini humo kwa mchezo wa kickboxing akiwa ndiye aliyeupa umaarufu.
Baada ya ushindi huo, Golola alitangaza kumtaka tena Mandonga ambaye amekuwa akimwita kwa jina la baba mdogo.
Katika pambano jingine, bondia mwingine Mtazania, Twaha Kiduku (pichani chini) naye alipoteza kwa pointi mbele ya Asemahle Wellem wa Afrika Kusini katika pambano la raundi 12 la kuwania mkanda wa WBF Inter Continental.

Wellem alitawala vyema pambano hilo na haikushangaza kushinda kwa pointi za majaji wote watatu huku akionekana kumzidi mpinzani wake kila eneo na hadi mwisho wa pambano, Kiduku alionekana kuwa na majeraha kadhaa usoni.
Hali ya wasiwasi ilijitokeza zaidi katika raundi ya tatu pale Wellem alipomshambulia Kiduku na ngumi ya ghafla ya mkono wa kushoto na bondia huyo kuanguka chini na mwamuzi kuanza kumhesabia.
Wellem ndio kwanza ameingia kwenye ngumi za kulipwa akitokea kwenye zile za ridhaa, katika ngumi za kulipwa ana rekodi ya mapambano sita yote akiwa ameshinda wakati Kiduku ana rekodi ya mapambano zaidi ya 20 hadi sasa.
