Madrid, Hispania
Real Madrid jana imepata ushindi mnono wa mabao 6-0 dhidi ya Levante, ushindi ambao umekuwa na maana kubwa kwa mfungaji wao mahiri Karim Benzema ambaye amefikisha rekodi ya mabao 323 iliyokuwa ikishikiliwa na Raul Gonzalez.
Katika mechi hiyo ya La Liga ambayo iliifanya Levante kushuka daraja baada ya kipigo hicho cha aibu, mabao ya washindi yalifungwa na Mendy dakika ya 13, Benzema dakika ya 19, Rodrygo dakika ya 34 na VinÃcius Júnior aliyepiga hat trick katika dakika za 45, 68 na 83.
Kwa Benzema, baada ya kuinasa rekodi ya Raul, sasa anakuwa mfungaji namba mbili mwenye mabao mengi katika klabu hiyo na kazi iliyobaki sasa kwake ni kuisaka rekodi ya mabao 450 ambayo inashikiliwa na Cristiano Ronaldo.
Benzema alijiunga na Real Madrid mwaka 2009 akitokea timu ya Lyon ya kwao Ufaransa wakati Raul ameichezea timu hiyo kwa mafanikio akiwa mfungaji tegemeo kuanzia mwaka 1994 hadi 2010.
Furaha nyingine katika ushindi wa jana ilikuwa kwa Vinicius ambaye alipiga hat trick ya kwanza katika klabu hiyo ambapo alisema, ” Ni hat trick yangu ya kwanza na wachezaji wenzangu wamekuwa wakinisaidia sana na nina furaha kweli kweli.”
Akimzungumzia Benzema, Vinicius alisema, “Sikuwa nikifahamu kama ameifikia rekodi ya Raul, amekuwa akifunga mabao mengi na kufanya mambo mengi kwa ajili ya timu.”
Real ambao ndio vinara wa La Liga, sasa wanasubiri kuumana na Cadiz, mechi itakayopigwa Jumapili ya wiki hii na kumalizia mechi nyingine ya ligi hiyo dhidi ya Real Betis hapo Mei 22 kabla ya kuisubiri Liverpool katika mechi ya fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya itakayopigwa Mei 28.
Kimataifa Benzema ainasa rekodi ya Raul
Benzema ainasa rekodi ya Raul
Read also
