Na mwandishi wetu
Beki mpya wa Singida Fountain Gate, Joash Onyango (pichani kulia) ameahidi kuipigania timu hiyo na kuipa mafanikio ambayo imedhamiria kuyapata msimu ujao.
Onyango, beki kutoka nchini Kenya, amejiunga na Singida kwa mkopo wa mwaka mmoja akitokea Simba SC.
Beki huyo ambaye amezungumza kwa mara ya kwanza tangu atue Singida hivi karibuni alisema sababu ya kuichagua Singida ni kutokana na mipango mizuri ya timu hiyo na ushiriki wao wa michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika msimu ujao.
“Nimejipanga kuhakikisha nashirikiana na wachezaji wenzangu kutimiza malengo ya timu msimu ujao katika mashindano yote ambayo tutashiriki,” alisema Onyango.
Beki huyo ambaye tayari ameanza mazoezi na kikosi cha timu hiyo alisema kwa muda mfupi aliojiunga na timu hiyo amepata ushirikiano wa kutosha kutoka kwa viongozi na wachezaji wenzake jambo ambalo limemuongezea ari ya kujituma zaidi.
Alisema anaamini uzoefu wa kutosha alionao katika ligi ya Tanzania utamsaidia na hakuna kitakachomshinda zaidi ya kutumia uzoefu wake kufanya vizuri.
Onyango aliyewahi pia kuwika na Gor Mahia ya Kenya, inaelezwa baadhi ya mambo yaliyomfanya atake kuondoka Simba, ni mashabiki wa timu hiyo kumshushia lawama kuwa anaifungisha timu hiyo katika michuano ya klabu Afrika hasa msimu uliopita.
