Sydney, Australia
Wakati Ujerumani ikiilaza Morocco mabao 6-0 na Brazil ikiichapa Panama 4-0, Jamaica inafurahia sare ya 0-0 mbele ya Ufaransa katika mechi za fainali za Kombe la Dunia za Wanawake zinazoendelea Australia na New Zealand.
Ujerumani ikiwa mjini Melbourne jana Jumatatu ilineemeka kwa mabao ya Alexandra Popp aliyefunga mawili, Klara Buhl na Lea Schüller pamoja na mabao mengine mawili ambayo wachezaji wa Morocco, Hanane Ait El Hajj na Yasmin Mrabet walijifunga.
Katika mechi hiyo Ujerumani iliwakosa wachezaji wake mahiri, Marina Hegering na Lena Oberdorf ambao ni majeruhi lakini ilifanikiwa kuanza vyema fainali hizo. Katika mechi zijazo Ujerumani itaivaa Colombia wakati Morocco itaikabili Korea Kusini.
Nayo Brazil katika mechi nyingine iliyopigwa jana ushindi wao dhidi ya Panama pia ulinogeshwa kwa rekodi ya hat trick (mabao matatu) yaliyofungwa na Ary Borges ambaye pia ndiye aliyetoa pasi iliyozaa bao la nne la timu hiyo lililofungwa na Bia Zaneratto.
Matokeo hayo yanaifanya Brazil kujiweka katika nafasi nzuri ya kusonga mbele katika Kundi F baada ya Ufaransa kuambulia sare ya 0-0 mbele ya Jamaica.
Naye kocha wa Jamaica, Lorne Donaldson akizungumzia sare ya timu yake dhidi ya Ufaransa alisema matokeo hayo yamekuwa ya kipekee kwao katika historia ya soka la wanawake kutokana na ubora wa wapinzani wao, Ufaransa.

Ufaransa inayonolewa na Herve Renard sasa inalazimika kukaa chini na kujipanga upya kabla ya mechi yao ya Julai 29 dhidi ya Brazil ambao ni wababe wengine wa soka la wanawake duniani.
Jamaica ambayo iko nyuma kwa nafasi 38 kwa Ufaransa kwa mujibu wa takwimu za Fifa, ilipambana vizuri na kupata matokeo hayo licha ya nahodha wa timu hiyo, Khadija Shaw kutolewa na kuifanya timu hiyo ibaki na wachezaji 10 uwanjani.
“Naweza kusema kwamba hadi sasa haya ni matokeo makubwa, namba moja, ni matokeo namba moja kwa timu ya wanawake na ya wanaume, ukiangalia tu takwimu za Fifa utayataja matokeo haya kuwa namba moja” alisema Donaldson.
Matokeo mechi za Kombe la Dunia Wanawake…
Colombia 2-0 Korea Kusini
New Zealand 0-1 Philippines
Ufaransa 0-0 Jamaica
Italia 1-0 Argentina
Ujerumani 6-0 Morocco
Brazil 4-0 Panama
Sweden 2-1 Afrika Kusini
Uholanzi 1-0 Ureno
