Riyadh, Saudi Arabia
Klabu ya Al Hilal ya Saudi Arabia inamtaka mshambuliaji wa PSG ya Ufaransa, Kylian Mbappe (pichani) na ipo tayari kuweka rekodi ya dunia kwa kumsajili kwa ada ya Pauni 259 milioni.
Mbappe ambaye pia ni nahodha wa timu ya Taifa ya Ufaransa ana uwezekano mdogo mno kuendelea kuichezea PSG msimu ujao wa 2023-24 unaoanza mapema mwezi ujao na tayari ameachwa na timu hiyo katika safari ya maandalizi ya msimu ujao nchini Japan.
Katika siku za karibuni amekuwa akihusishwa zaidi na mipango ya kujiunga na klabu ya Real Madrid ya Hispania kabla ya Al Hilal kumtangazia ofa mpya kubwa hii leo Jumatatu.
Mbappe amebakiza mwaka mmoja katika mkataba wake wa sasa na PSG na ameshaweka wazi msimamo wake wa kubaki katika klabu hiyo lakini hataki kusaini mkataba mpya wakati huu.
Msimamo huo unapingana na msimamo wa Rais wa PSG, Nasser Al Khelaifi ambaye amemtaka mchezaji huyo achague moja kama anataka kubaki PSG lazima asaini mkataba mpya wakati huu tofauti na hivyo aondoke.
Mbappe mwenye umri wa miaka 24 alijiunga na PSG mwaka 2017 akitokea Monaco kwa ada ya Pauni 166 milioni na tangu wakati huo amekuwa mfungaji tegemeo wa mabao wa timu pamoja na timu ya Taifa ya Ufaransa.
Mchezaji wa mwisho kusajiliwa PSG kwa bei mbaya alikuwa ni Neymar ambaye ada yake ilifikia Pauni 200 milioni mwaka 2017 akitokea Barcelona na kama mpango wa Al Hilal utafanikiwa basi usajili wa Mbappe katika klabu hiyo itakuwa rekodi nyingine ya dunia lakini pia utamfanya Mbappe aungane na mastaa wengine wa soka waliowahi kutamba Ulaya na kwa sasa wanacheza soka Saudi Arabia kina Cristiano Ronaldo, Karim Benzema, Eduardo Mendy na wengineo.
Kimataifa Al Hilal ya Saudi Arabia yamtaka Mbappe
Al Hilal ya Saudi Arabia yamtaka Mbappe
Read also
