Na mwandishi wetu
Kipa namba moja wa Simba, Aishi Manula ambaye atakuwa nje ya uwanja kwa miezi minne ameanza kujifua kwa mazoezi mepesi akiwa gym.
Manula ambaye amefanyiwa upasuaji wa nyama za paja, ameanza mazoezi hayo juzi akionekana kuchechemea kwa kujivuta akitumia mpira maalum wa kujifunga miguuni na kujaribu kupiga nao hatua.
Kipa huyo ambaye pia anaichezea timu ya taifa, Taifa Stars, pia akiwa mazoezini hapo alisema kwa kifupi tayari ameanza kupiga hatua kurejea kazini akimaanisha kurejea kuitumikia Simba.
Manula alipata majeraha hayo Aprili 7 katika mechi ya robo fainali ya Kombe la FA (ASFC) dhidi ya Ihefu kwenye Uwanja wa Mkapa, Dar es Salaam na kisha kufanyiwa upasuaji Mei 30, mwaka huu nchini Afrika Kusini.
Kuelekea msimu ujao, Simba ambayo pia imeondokewa na kipa wake namba mbili, Beno Kakolanya, inaendelea na mipango ya kumnasa kipa Mcameroon, Medjo Omossola kutoka Saint-Eloi Lupopo ya DR Congo.
Soka Manula aanza mazoezi mepesi
Manula aanza mazoezi mepesi
Read also
