Na mwandishi wetu
Nyota wa Simba, Clatous Chama na kiungo mpya wa timu hiyo, Fabrice Ngoma kesho Ijumaa wanatarajia kuungana na wachezaji wenzao mazoezini nchini Uturuki.
Wachezaji hao waliondoka Dar es Salaam, alfajiri ya leo kwa ajili ya kuungana na wenzao kwenye kambi hiyo ya wiki tatu ambayo inatarajiwa kuvunjwa Julai 31, mwaka huu.
Chama hakusafiri na wenzake kutokana na kuwa na madai yake ya kuomba aboreshewe maslahi kwenye mkataba wake na baada ya kukutana na kumalizana na uongozi wa Simba, mchezaji huyo amekubali kwenda kambini kujiunga na wenzake.
Meneja Habari na Mawasiliano Simba, Ahmed Ally alisema nyota hao walitarajiwa kuwasili Uturuki jioni na kesho asubuhi wataungana na wenzao kwenye mazoezi.
“Chama na Ngoma kesho wataanza mazoezi na wenzao baada ya kuondoka nchini alfajiri ya leo na kutarajiwa kuwasili Uturuki jioni,” alisema Ally ambaye alieleza kuwa maandalizi yao yanakwenda vizuri na kikosi chao kinafanya mazoezi mara mbili kwa siku asubuhi na jioni.
Ally pia alisema kwamba baada ya idadi kubwa ya wachezaji wao kuwasili kambini wanatarajia kuanza kucheza mechi za kirafiki.
Alisema wamepanga kucheza mechi tatu hadi nne za kirafiki lakini hiyo itategemea na muda kama utawaruhusu pamoja na kupata timu za kucheza nazo.
Soka Chama, Ngoma waelekea Uturuki
Chama, Ngoma waelekea Uturuki
Read also
