Na mwandishi wetu
Yanga jana imemtambulisha winga wa kushoto wa Marumo Gallants ya Afrika Kusini, Mahlatse Makudubela ‘Skudu’ (pichani) huku baadhi ya wadau wakiamini uzoefu wa mchezaji huyo unaweza kuisaidia timu hiyo kimataifa.
Wakizungumza na GreenSports kwa nyakati tofauti baadhi ya makocha wazawa; Kenny Mwaisabula, Juma Mwambusi, Charles Mkwasa wamezungumzia usajili huo uliokuwa ukisubiriwa kwa hamu hasa baada ya kuelezwa ndiye aliyerithi namba ya kiungo Feisal Salum ‘Fei Toto’ aliyetimkia Azam.
Mwaisabula alisema anaamini Yanga imemchagua mchezaji huyo ambaye ni mtu mzima kwa umri, (miaka 33) kutokana na uzoefu kwani anaweza kuwasaidia hasa katika mechi za kimataifa.
Alikwenda mbali akijaribu kumfananisha kwa ubora na mchezaji wa zamani wa Majimaji, Pamba na Yanga aliyefahamika kama Celestine Mbunga ‘Sikinde’ akisema huenda anaweza kuwa kama huyo.
“Kwa namna nilivyomuona akiwa na Marumo Gallants ni kama Celestine Sikinde, alikuwa winga hatari hivyo, kama atafanya kama nilivyomuona atawasaidia mno,”alisema.

Kwa upande wake, kocha wa zamani wa Mbeya City, Yanga na Azam, Juma Mwambusi alisema huenda Yanga kuna kitu walikiona kwa mchezaji huyo kinachoweza kuwasaidia katika michuano watakayoshiriki msimu ujao.
“Hatuwezi kubeza kwa sababu ni lazima tumuone, naamini wamesajili kulingana na taarifa za benchi la ufundi lililopita, na kama kuna kitu walikiona kwake atawasaidia kuziba mapungufu wanayoyaona,” alisema.
Kocha wa zamani wa Taifa Stars, Charles Boniface Mkwasa alisema mchezaji huyo kwanza anatoka katika ligi yenye ushindani nchini Afrika Kusini, hivyo kwa maana nyingine huenda akaleta kitu tofauti katika soka nchini.
Ingawa alieleza wasiwasi wake kuwa licha ya uzuri wa mchezaji huyo lakini umri alionao huenda hatokuwa na muda mrefu katika soka, hivyo akatumika kidogo na Wanajangwani hao.
Naye mchambuzi wa soka nchini, Dominic Salamba alisema Yanga ilikuwa na udhaifu wa kupata mabao ya pembeni hivyo usajili wa winga huyo huenda utasaidia kuongeza kasi na ufungaji wa mabao mengi yanayotoka pembeni.
“Yanga ilikuwa inapata shida kufunga mabao ya pembeni ndio maana hata magoli yao yalikuwa machache na mpira wa kisasa unahitaji magoli mengi yanayotoka pembeni, kwa hiyo ujio wa Skudu pengine ataongeza ubunifu, na pia ana mbinu ambazo wachezaji wengi wa Tanzania hawana,” alisema Salamba..
Skudu amewahi kucheza klabu mbalimbali zikiwemo United FC, Platnum Stars, Golden Arrows, Chippa United, Orlando Pirates, Highland Parks na University of Pretoria.
Huo ni usajili mpya wa tano kwa Yanga baada ya Nickson Kibabage kutoka Singida Fountain Gate, Max Nzengeli kutoka AS Maniema ya DR Congo, Yao Attohoula (Asec Mimosas), Jonas Mkude (Simba) na Gift Fred aliyekuwa SC Villa ya Uganda.
