Na mwandishi wetu
Ikiwa ni wiki moja tangu aanze mazoezi baada ya kusajiliwa Yanga, kiungo mpya wa timu hiyo, Jonas Mkude amemmwagia sifa Kocha Mkuu, Miguel Gamondi akisema mazoezi yake yamemfanya awe mwepesi na kuwa tayari kwa mapambano.
Mkude ametua Yanga msimu huu akitokea kwa watani zao Simba, timu ambayo ameitumikia kwa takriban miaka 13 na kupata nayo mafanikio kadhaa.
Akizungumza kwa mara ya kwanza tangu atue kwa mabingwa hao watetezi wa Ligi Kuu NBC, Mkude alisema kwa siku chache ambazo amefanya kazi na kocha huyo ameona mabadiliko makubwa katika mwili wake jambo ambalo analifurahia.
“Nafurahi kuona kocha, wachezaji wenzangu na hata mashabiki wamenipokea vizuri tofauti na nilivyokuwa nafikiria, hii imenipa nguvu ya kuzidi kujituma ukichanganya na mazoezi ambayo tumekuwa tukiyafanya naamini nitakuwa na mwanzo mzuri nikiwa na Yanga,” alisema Mkude maarufu Nungunungu.
Kiungo huyo alieleza kuwa yupo Yanga kwa ajili ya kufanya kazi na kutimiza malengo ambayo wamejiwekea kuelekea msimu ujao, hivyo mashabiki wao hawapaswi kuwa na hofu naye kwani atahakikisha anawapa furaha kwa kushirikiana na wachezaji wenzake.
Alisema anajua kuwa amejiunga na timu kubwa yenye malengo makubwa hasa kwenye mashindano ya kimataifa, hivyo atahakikisha anatumia uzoefu aliokuwa nao kuisaidia timu yao ifike pale walipo kusudia.
Mkude anatarajiwa kupata upinzani mkali kwenye eneo la kiungo la Yanga, hasa kutokana na uwepo wa Khalid Aucho na Yannick Bangala ambao wamefanya vizuri na kuipa mafanikio makubwa timu hiyo kwenye misimu miwili iliyopita.
Soka Mkude amkubali Gamondi
Mkude amkubali Gamondi
Read also
