Na mwandishi wetu
Klabu ya Simba inatarajia kufunga zoezi la usajili kwa kumsajili kipa, Medjo Simon Loti Omossola (pichani) kutoka timu ya Saint-Eloi Lupopo ya DR Congo.
Simba inasaka kipa atakayeziba pengo la Aishi Manula ambaye kwa sasa anauguza majeraha ya goti baada ya kufanyiwa upasuaji wiki nne zilizopita na atakuwa nje hadi mwishoni mwa Oktoba, mwaka huu.
Meneja Habari na Mawasiliano wa Simba, Ahmed Ally alisema wapo katika hatua za mwisho kukamilisha usajili wa kipa huyo ambaye wanaamini atakuwa mbadala sahihi wa Manula hasa kutokana na uzoefu wake kwenye mashindano ya kimataifa.
“Simon ni nyanda wa viwango kwelikweli na hiyo ni kutokana na uzoefu aliokuwa nao baada ya kupita klabu mbalimbali ambazo ni kubwa na zimekuwa na desturi ya kushiriki michuano ya kimataifa mara kwa mara, huyu ndio tutafunga naye usajili wetu katika dirisha hili kubwa,” alisema Ally.
Ally alisema usajili wao wa msimu huu umezingatia vitu vingi ikiwemo ubora wa mchezaji husika na mchango wake kwenye timu anayotokea na kipa huyo amekidhi vigezo ndio maana wameamua kumchukua ili kuongeza thamani kwenye kikosi chao cha msimu ujao.
Alisema kupata saini ya Simon ambaye ni raia wa Cameroon kunaifanya safu yao ya ulinzi kuwa salama kama ilivyokuwa wakati wa Manula kabla hajapata majeraha yanayomweka nje kwa muda mrefu.
Awali Simba ilipanga kumsajili kipa Caique da Santos raia wa Brazil ambaye lilikuwa pendekezo la kocha Roberto Oliveira ‘Robertinho’ lakini ilibadili mawazo na kuachana naye.
Sababu kubwa ya kuachana na kipa huyo ikielezwa ni kutokana na kuzungumza ya Kireno pekee, kitu ambacho kingemsumbua katika kuwasiliana na wachezaji wenzake.
Soka Kipa wa Lupopo kufunga usajili Simba
Kipa wa Lupopo kufunga usajili Simba
Read also
