Abidjan, Ivory Coast
Rais wa Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa) Gianni Infantino amesema ligi ya soka ya timu nane bora za Afrika maarufu Super League ambayo timu ya Simba itashiriki, itaanza Oktoba 20 mwaka huu.
Infantino (pichani) ametoa kauli hiyo jana Alhamisi kwenye mkutano mkuu wa Shirikisho la Soka Afrika (CAF) uliofanyika mjini Abidjan, Ivory Coast na kuongeza kuwa mpango uliopo ni kuiboresha zaidi ligi hiyo.
Mpango wa awali ulikuwa ni kushirikisha jumla ya timu 24 za Afrika lakini baadaye makubaliano yalifikiwa na idadi ya timu kupunguzwa hadi kufikia nane.
“Ligi itahusisha timu nane bora na baadaye itafuatiwa na mpango mkubwa zaidi, ni lazima tuwekeze kwenye klabu za soka za Afrika pamoja na timu za soka za Taifa,” alisema Infantino mbele ya wajumbe wa mkutano huo.
“Ni jukumu na wajibu wetu na kwa kushirikiana wote kwa pamoja tukiwa kama timu tutafanikiwa katika hilo,” aliongeza Infantino.
Kwa mujibu wa CAF, michuano ya Super Ligi itafanyika sambamba na Ligi ya Mabingwa Afrika na kwamba Super Ligi haijaanzishwa kuwa mbadala wa Ligi ya Mabingwa Afrika kama inavyodhaniwa
Kwa upande wake Rais wa CAF, Patrice Motsepe akiizungumzia ligi hiyo alisema kuna ulazima wa kuliboresha soka la Afrika na kulipa nguvu na mvuto zaidi duniani na ligi hiyo imeanzishwa ili kufikia malengo hayo.
Motsepe pia aliwataka viongozi wa mashirikisho ya soka Afrika pamoja na serikali za Afrika kuhakikisha zinawekeza zaidi kwenye mchezo wa soka.
“Tuna imani kubwa kwamba mafanikio tunayoyapata na vipaji vilivyopo Afrika matokeo yanaweza kuwa Afrika kushinda Kombe la Dunia, lakini lazima tutumie fedha kuwafundisha makocha, kufungua akademi na kuhakikisha klabu za soka zinakuwa na rasilimali za kutosha,” alisema Motsepe.
Ukiacha Simba ya Tanzania, timu nyingine zinazotajwa kushiriki ligi hiyo ni Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini, Petro Atletico (Angola), Al Ahly (Misri), Wydad Casablanca (Morocco), TP Mazembe (DR Congo), Esperence (Tunisia) na Horoya (Guinea).
