Na mwandishi wetu
Azam FC imeeleza kuelemewa na ratiba inayowafanya washindwe kupanga siku maalum ya tamasha la Azamka linalotumika kutambulisha wachezaji wao wapya kuelekea msimu ujao.
Ofisa Habari wa Azam, Zakaria Thabiti ameiambia GreenSports kuwa wanashindwa kufahamu ni lini watafanya tamasha hilo kwa kuwa watachelewa kurejea kutoka Tunisia walikokwenda kuweka kambi, wakirudi watakuwa wanakabiliwa na mechi za Ngao ya Jamii.
“Timu itarejea mwisho wa mwezi Julai, kwa hiyo kuanzia tarehe moja Agosti tutakuwa nchini lakini tarehe 4 ya mwezi huo tutakuwa na mechi za timu za taifa za kufuzu Chan (michuano ya Afrika kwa wachezaji wa ndani)…
“Na sisi tunaweza kuwa waathirika sababu wachezaji wanaweza wakaitwa, kwa hiyo tukitangaza hapo kuna wengine tutawakosa, wakirudi tu kidogo tayari kuna mechi za Ngao ya Jamii kuanzia tarehe 8, kwa hiyo tunapasua kichwa tufanyaje hili tamasha,” alisema Zakaria.
Alisema lengo lao ni kuwatambulisha kwa mashabiki kabla ya kucheza mechi rasmi hata moja hivyo wanatazama kwa kina ni lini wafanye hivyo kati ya Agosti mosi mpaka 7, mwaka huu lakini bado nafasi hiyo ni finyu mno.
Azam FC imetangaza kufunga usajili baada ya kuwanasa Feisal Salum ‘Fei Toto’ kutoka Yanga, Mgambia, Djibril Sillah aliyekuwa Raja Casablanca, Cheikh Sidibe (Teungueth) na Allasane Diao (US Goree) ambao wote ni raia wa Senegal.
Soka Ratiba yaiweka pagumu Azamka
Ratiba yaiweka pagumu Azamka
Read also
