Na mwandishi wetu
Siku moja baada ya beki wa kati ya Simba, Joash Onyango kuuzwa kwa mkopo Singida Fountain Gate, klabu hiyo leo Jumapili imetangaza kumsajili beki mpya wa kati, Che Malone Fondoh kutoka Coton Sport ya Cameroon.
Fondoh (pichani) anatarajiwa kuwa ndiye atakayecheza beki ya kati ya Simba na Henock Inonga ambaye kwa muda mrefu amekuwa akicheza katika eneo hilo na Onyango.
Beki huyo ambaye anatumia zaidi mguu wa kulia licha ya kucheza vizuri katika nafasi ya beki ya kati, pia humudu beki ya kulia hivyo anaweza kuwa msaada kwa Simba katika eneo hilo kukiwa na ulazima.
Fondoh ambaye amesaini mkataba wa miaka miwili pia ni nahodha msaidizi wa timu ya Taifa ya Cameroon inayoshiriki michuano ya Mataifa ya Afrika kwa wachezaji wa ndani yaan CHAN.
Beki huyo anakuwa mchezaji wa pili kutoka Cameroon kusajiliwa na Simba katika siku za karibuni, aliyemtangulia Fondoh ni kiungo mshambuliaji, Willy Essomba Onana.
Fondoh mwenye umri wa miaka 24 anatajwa kuwa ni sehemu ya mpango maalum wa klabu ya Simba kuhakikisha inafanya vizuri msimu ujao hasa kwenye mashindano ya kimataifa ambapo timu hiyo itashiriki Ligi ya Mabingwa Afrika.
Msimu uliopita Simba iliishia hatua ya robo fainali ya michuano hiyo, na mkakati uliopo sasa mbali na kuhakikisha wanafanya vizuri katika mashindano ya ndani, pia wamepania kutamba kimataifa.
Soka Simba yapata mrithi wa Onyango
Simba yapata mrithi wa Onyango
Read also
