Na mwandishi wetu
Klabu ya Azam FC, imeeleza kuwa mshambuliaji Msenegali, Alassane Diao waliyemsajili kutoka US Goree walimchukua akiwa huru na hakuwa na mkataba na klabu ya Goree kama inavyoelezwa.
Azam imeeleza hayo baada ya Goree juzi kutoa taarifa kwa umma kuwa Diao ni mchezaji wao halali na amesajiliwa akiwa na mkataba na timu hiyo, hivyo wanajipanga kuchukua hatua stahiki.
Ofisa Habari wa Azam, Zakaria Thabit (pichani juu) amezungumza na GreenSports na kusema kwanza wao hawana taarifa rasmi za malalamiko hayo zaidi ya kuona mitandaoni lakini wana nyaraka zote sahihi zinazoonesha mchezaji huyo alikuwa huru wakati wanamsajili.
“Kama kweli wana mkataba naye walete malalamiko rasmi kwetu, pili tulishawasiliana na kambi ya mchezaji na kuthibitisha juu ya kumalizika kwa makataba wake. Isipokuwa mkanganyiko uliopo umetokana na kusogezwa mbele kwa msimu wa ligi ya Senegal.
“Kilichotokea ni ligi yao kusogezwa mbele na kufanya mkataba wa Diao kumalizika kabla ya ligi kuisha, wao walipaswa wamwombe mchezaji amalizie ligi wakati huu lakini wanasema ni mchezaji wao halali wakati kimsingi amemaliza mkataba,” alisema Zakaria.
Ligi Kuu ya Senegal maarufu Ligue 1 inayoshirikisha timu 14 mpaka sasa imecheza mechi 23 zikiwa zimesalia mechi tatu kabla ya kufungwa rasmi kwa pazia la ligi hiyo msimu huu.
