Na mwandishi wetu
Siku chache baada ya Azam FC kumtangaza mshambuliaji Alassane Diao, klabu ya US Goree ya Senegal aliyotokea mchezaji huyo imeeleza kusikitishwa na Azam kumsajili Diao wakati wao wana mkataba naye.
Goree imeeleza hayo kupitia taarifa waliyoweka juzi kwenye mtandao wao wamedai kuwa kutokana na hayo wamedhamiria kufuata sheria za uhamisho zilizowekwa na Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa).
Katika hilo, klabu ya US Goree imedhamiria kuhakikisha maslahi ya klabu na wachezaji wake chini ya mkataba yanazingatiwa.
“Kupitia mitandao ya kijamii, Union Sportive Goreenne imebaini utiaji saini wa mkataba wa miaka miwili kati ya mchezaji wetu Alassane Diao na klabu ya Azam FC ya Tanzania.
“Diao bado ana mkataba na US Goree, na hakuna mazungumzo yoyote yaliyoanzishwa na klabu ya Azam FC katika mwelekeo wa kumwachilia mchezaji huyo hivyo hawezi kufuzu kucheza katika klabu nyingine Senegal au kimataifa kabla ya mwisho wa mkataba wake wa sasa.
“Kwa kuheshimu taratibu zinazosimamia soka, US Gorée inasisitiza dhamira yake ya kufuata sheria za uhamisho zilizowekwa na Fifa na kuhakikisha maslahi ya klabu na wachezaji wake walio chini ya mkataba,” ilieleza taarifa hiyo iliyowekwa juzi na uongozi wa Goree.
GreenSports ilifanya juhudi za kumtafuta Mtendaji Mkuu wa Azam FC, Abdulkarim Amin ‘Popat’ kuhusiana na sakata la mchezaji huyo raia wa Senegal lakini simu yake muda wote ilikuwa ikitumika.
Hata alipotafutwa Ofisa Habari wa Azam, Zakaria Thabiti ili atoe ufafanuzi wa jambo hilo naye simu yake ya mkononi iliita bila ya kupokelewa.
Soka Diao kuiingiza matatani Azam FC?
Diao kuiingiza matatani Azam FC?
Read also
