London, England
Kiungo Granit Xhaka ameihama Arsenal na kujiunga na klabu ya Bayer Leverkusen ya Ujerumani kwa mkataba wa miaka mitano na ada ya dola 21 milioni.
Xhaka mwenye umri wa miaka 30 ambaye alijiunga Arsenal mwaka 2016 na kuwa nahodha wa timu hiyo kwa muda mfupi mwaka 2019, alikuwa amebakiza mwaka mmoja katika mkataba wake Arsenal.
Arsenal kwa sasa inapambana kwa hali na mali kuinasa saini ya kiungo wa West Ham na England, Declan Rice ambaye pia anawaniwa na Man City na huenda akaweka rekodi ya uhamisho kwa Uingereza.
Xhaka hadi anaondoka Arsenal ana rekodi ya kuifungia timu hiyo mabao 23 katika mechi 297 na ameiwezesha kubeba taji la FA mara mbili na kumaliza nafasi ya pili katika Ligi Kuu England (EPL) msimu uliopita wa 2022-23.
Alifunga mabao mawili katika ushindi wa mabao 5-0 ambao Arsenal iliupata katika mechi ya mwisho ya EPL dhidi ya Wolves kabla ya kufanyiwa mabadiliko na wakati akitoka mashabiki walisimama na kumpa heshima.
Hali hiyo imekuwa tofauti na kilichowahi kumtokea siku za nyuma baada ya kugombana na mashabiki wa Arsenal wakati alipofanyiwa mabadiliko katika mechi dhidi ya Crystal Palace Oktoba 2019.
Katika tukio hilo, Xhaka alionesha hasira za kutolewa na kukiri kwamba alikaribia kuondoka Arsenal ambapo baadaye alivuliwa unahodha ikiwa ni kama mwezi mmoja baada ya kupewa cheo hicho na aliyekuwa kocha wa Arsenal wakati huo, Unai Emery.
Mwaka 2021, Arsenal ilikataa kumuuza Xhaka katika klabu ya Roma kwa ada ya Pauni 12.9 milioni na baadaye katika kipindi hicho hicho cha majira ya kiangazi akasaini mkataba wa mwaka mmoja zaidi ambao ulitakiwa kufikia ukomo mwaka 2024.
Kabla ya kutua Arsenal, Xhaka alikuwa akiichezea Borussia Monchengladbach pia ya Ujerumani, klabu ambayo ilimuuza Arsenal kwa ada inayodaiwa kufikia Pauni 35 milioni.
Kimataifa Granit Xhaka aondoka Arsenal
Granit Xhaka aondoka Arsenal
Read also
