Na mwandishi wetu
Klabu ya Yanga imeeleza kuwa itamfanyia vipimo zaidi vya kitabibu mshambuliaji wao, Denis Nkane ili kujua iwapo ameathirika zaidi maeneo ya kichwani.
Hiyo ni baada ya mchezaji huyo kudondoka chini na kufikia kichwa wakati akiwania mpira kwenye mechi ya kirafiki dhidi ya Nyasa Big Bullets ya Malawi iliyopigwa kwenye Uwanja wa Bingu, Lilongwe nchini Malawi.
Akizungumza na GreenSports, Ofisa Habari wa Yanga, Ali Kamwe alisema kuwa mchezaji huyo licha ya kupoteza fahamu baada ya kudondoka, baadaye alizinduka na kuendelea na shughuli nyingine ndogondogo ingawa madaktari walieleza kuchukuliwa vipimo zaidi mchezaji huyo baada ya kurejea Dar es Salaam.
“Kwa jitihada kubwa Nkane alipata huduma ya kwanza na akarejesha fahamu zake kama kawaida, lakini madaktari wameshauri kwamba tukifika Dar es Salaam tufanye vipimo zaidi kuona kama amepata majeraha mengine,” alisema Kamwe.
“Hali yake ina ahueni yuko vizuri sasa hivi anaongea na wenzake, anakula japo ana maumivu ya kichwa, kwa hiyo tukirudi tutaangalia kipimo kikubwa zaidi kuangalia kama ana majeraha mengine au vipi kwa ajili ya usalama zaidi,” alisema Kamwe.
Tayari kikosi hicho cha mabingwa wa Ligi Kuu NBC kimewasili nchini jana usiku kikitarajiwa kuanza kuingia kambini Avic Town Julai 10, mwaka huu tayari kwa kuanza maandalizi rasmi ya msimu ujao wa 2023-24.
