London, England
Mshambuliaji wa Arsenal, Gabriel Jesus amesema aliamua kuondoka Man City baada ya kocha Pep Guardiola kumfanya alie alipomtoa kwenye kikosi cha kwanza katika mechi ya Ligi ya Mabingwa Ulaya.
Jesus alikuwa Man City chini ya Pep kwa takriban miaka mitano kabla ya kuhamia Arsenal majira ya kiangazi mwaka jana, uhamisho ambao anasema ulimfanya ajione yuko huru.
Akizungumza katika mahojiano hivi karibuni, Jesus alisema mambo yake yalibadilika Man City katika mechi ya nyumbani ya Ligi ya Mabingwa Ulaya mwaka 2021 dhidi ya Paris Saint-Germain (PSG) alipotajwa katika orodha ya wachezaji walioanzia benchi.
“Kulikuwa na mechi ya Ligi ya Mabingwa Ulaya dhidi ya PSG kwenye uwanja wa nyumbani, Pep alimpa nafasi Zinchenko acheze namba 9 feki, jambo la ajabu,” alisema Jesus.
“Siku moja kabla hakuwahi hata kumtumia Zinchenko mazoezini, alinipanga mimi katika nafasi ya ushambuliaji, Zinchenko alifikia hatua hadi ya kunidhihaki kwamba siku ile alinionea huruma,” aliongeza Jesus.
“Saa mbili kabla ya mechi kulikuwa na mazungumzo ya timu, kula pamoja, kupumzika kwa dakika 30 na kwenda kwenye mechi, na ndipo akaitaja timu, kwa kweli sikuweza kula nilikwenda moja kwa moja chumbani huku nikilia, nilimpigia simu mama na kuzungumza naye, nilimwambia nataka kuondoka, narudi nyumbani kwa sababu amempanga, Zinchenko, hakunipanga mimi, amempanga beki wa kushoto, ni ukichaa,” alisema.
Jesus baadaye aliingia kuchukua nafasi ya Zinchenko kipindi cha pili na kutoa pasi iliyozaa bao la kusawazisha kabla ya kufunga bao la ushindi na mpira kumalizika kwa City kutoka na ushindi wa 2-1.
“Sikufanya mazoezi ya kupasha misuli, nilijisikia vibaya, dakika tano baada ya Mbappe (Kylian) kufunga bao na sisi kuwa nyuma kwa bao 1-0, Pep aliniingiza, nikatoa pasi na kufunga matokeo yakawa 2-1, mechi iliyofuata dhidi ya RB Leipzig nilidhani atanipanga, hakunipanga, haikuwa rahisi nikaamua kuondoka,” alisema Jesus.
Jesus alijiunga na Man City Januari 2017 akitokea klabu ya Palmeiras ya Brazil na akiwa City ameweza kubeba mataji 11 na timu hiyo.
