Na mwandishi wetu
Bondia Hassan Mwakinyo anatarajia kupanda ulingoni kuwania mkanda wa Dunia wa WBO kwa mara ya kwanza katika pambano linalotarajiwa kupigwa mwezi Agosti, mwaka huu.
Mwakinyo ambaye mara ya mwisho kupanda ulingoni ilikuwa Septemba, mwaka jana alipopoteza pambano dhidi ya Liam Smith mjini Liverpool kwa TKO, safari hii atapanda ulingoni chini ya Kampuni ya ngumi ya PAF Promotion Entertainment.
Mwakinyo alisema kuwa kwa sasa amejipanga kuhakikisha anakata kiu ya Watanzania katika mchezo wa ngumi za kulipwa kwa kucheza pambano la mkanda ambao hajauwahi kuchezwa nchini huku mpinzani wake akitarajia kutangazwa baadae.
“Baada ya kukosekana ulingoni katika ngumi za ushindani kwa muda mrefu nawashukuru ndugu zangu waandishi kwa kuja hapa natarajia kupanda ulingoni mwezi ujao katika pambano kubwa la kuwania mkanda wa Ubingwa wa Dunia wa WBO.
“Muda mrefu nilikuwa natamani nipate pambano kama hili lakini nilikua bado sina vigezo, sasa nashukuru nimevipata na utakua wakati mzuri sana kwangu kupata pambano hili. Ningefurahi pia mabondia wa Tanzania wangepata na wao nafasi kama hii tena wakipigana hapahapa nchini lakini bado vigezo hawana,” alisema Mwakinyo.
Mwakinyo alifafanua kwamba ukimya wake haukuwa wa bure na amejiweka sawa vilivyo kukidhi kiu ya mashabiki wake ambao hawajamuona muda mrefu ulingoni ambapo amepania kuwaburudisha siku ya pambano hilo.
Mwakinyo pia alisema: “Kwa bondia wa Tanzania yeyote anayetaka kupigana na mimi, kwanza agombee mkanda huu ninaokwenda kuupigania. Lakini pia hata mabondia wakubwa huwa wanacheza ‘sparring’ hivyo kama kuna bondia anataka hivyo aje Masaki tupigane.” alisema Mwakinyo.
