Rio de Janeiro, Brazil
Mamlaka nchini Brazil zimemtoza faini ya Dola 3.3 milioni mshambuliaji wa PSG, Neymar kwa kosa la kuharibu mazingira katika ujenzi wa mjengo wake wa kifahari uliopo pwani ya mji wa Mangaratiba nje kidogo ya jiji maarufu la Rio de Janeiro.
Kwa mujibu wa taarifa ya mamlaka za mji wa Mangaratiba, Neymar ameadhibiwa kwa kosa la kujenga bwawa lisilo rasmi katika mjengo wake kwenye pwani hiyo jambo ambalo ni kinyume na sheria za mazingira.
Neymar ana haki ya kukata rufaa adhabu hiyo lakini watu wake hawakuwa tayari kuzungumza lolote kama wataamua kulipa faini hiyo au watakata rufaa.
Adhabu hiyo imekuja ikiwa ni takriban siku 10 zimepita baada ya maofisa wa idara ya mazingira kufanya ukaguzi katika mjengo wa Neymar na kukuta ujenzi mkubwa ukiendelea bila ya kibali cha mamlaka za usimamizi wa mazingira.
Kwa mujibu wa maofisa wa idara ya mazingira katika ujenzi huo kuna uharibifu mkubwa uliofanywa katika pwani hiyo ikiwamo kuchepusha maji ya ziwa pamoja na uharibifu wa uoto wa asili.
“Idara ya Mazingira mbali na kutoza faini pia kwa kuzingatia uharibifu uliofanyika na kutoheshimu sheria za mazingira imewasilisha tukio hilo kwa ofisi ya mwendesha mashitaka, polisi na bodi nyingine zinazohusika na usimamizi wa mazingira,” ilieleza taarifa ya mamlaka ya mji wa Mangaratiba.
Habari zaidi zinadai kwamba Neymar da Silva Santos ambaye ni baba mzazi wa Neymar aliwatolea maneno makali maofisa wa idara ya mazingira waliofika kukagua ujenzi wa mjengo wa mtoto wake.
Sehemu ya bwawa ambalo Neymar anadaiwa kujenga lina ukubwa wa mita za mraba 1,000 na hadi maofisa wa mazingira wanafanya ukaguzi wao tayari mchezaji huyo alikuwa ametumia zaidi ya Dola 25,000 katika ujenzi huo.
