Riyadh, Saudi Arabia
Nahodha wa zamani wa timu ya Liverpool, Steven Gerrard (pichani) ametangazwa kuwa kocha wa klabu ya Al-Ettifaq ya Saudi Arabia licha ya awali kudai kwamba asingekuwa tayari kufanya kazi nchini humo.
Mapema mwezi uliopita, Gerrard alisema kwamba amepata ofa ya kufanya kazi ya ukocha katika klabu ya Saudi Arabia lakini aliamua kuikataa ofa hiyo.
Gerrard amesaini mkataba wa miaka miwili na klabu hiyo inayoshiriki Ligi Kuu Saudi Arabia baada ya kuwa bila ya kazi tangu Oktoba mwaka jana alipotimuliwa Aston Villa kutokana na mwenendo mbaya.
Al-Ettifaq inashiriki Ligi Kuu Saudi Arabia, ligi ambayo ina jumla ya timu 16 na msimu uliopita, ilimaliza ligi hiyo ikiwa nafasi ya saba nyuma ya vinara Al-Ittihad kwa tofauti ya pointi 35.
“Hakuna ubishi kwamba uwapo wa Gerarrd utakuwa kitu cha ziada katika kutuinua kwenye ligi yetu,” alisema Khalid Al-Dabal, mwenyekiti wa klabu ya Al-Ettifaq.
Gerrard ambaye pia amewahi kutamba na timu ya Taifa ya England, ni jina jingine kubwa katika soka la Saudi Arabia baada ya hivi karibuni kushuhudiwa wachezaji mastaa wa Ulaya wakijiunga na timu za nchini humo.
Wachezaji hao ni Cristiano Ronaldo aliyejiunga na klabu ya Al-Nassr Januari mwaka huu na kufuatiwa na Karim Benzema, Edouard Mendy, Ruben Neves, Kalidou Koulibaly na N’Golo Kante.
Wakati huo huo zipo habari kwamba baada ya kumpata Gerrard, Al-Ettifaq pia inajiandaa kuwasajili kiungo wa Liverpool, Jordan Henderson na mshambuliaji wa Chelsea, Pierre-Emerick Aubameyang.
Kimataifa Steven Gerrard kocha mpya Al-Ettifaq
Steven Gerrard kocha mpya Al-Ettifaq
Read also
