Na mwandishi wetu
Klabu ya Yanga imeingia mkataba wa miaka miwili na Benki ya NMB kwa ajili ya ushirikiano katika maeneo manne ambayo ni usajili wa wananchama na mashabiki, miundombinu, biashara na kimfumo ingawa haikuelezwa mkataba huo una thamani ya shilingi ngapi.
Akizungumza kwenye mkutano na waandishi wa habari uliofanyika Makao Makuu ya NMB, Dar es Salaam leo Jumamosi, Rais wa Yanga, Hersi Said alisema katika kipindi hicho cha miaka miwili wanachama wao wanatarajia kunufaika kwa mambo mengi kupitia ushirikiano huo.
Ameeleza namna ambavyo mashabiki na wanachama watanufaika ikiwa ni sehemu ya utatuzi wa changamoto ambazo zilikuwa zikiwasumbua kwenye mfumo wa usajili wa kidijiti.
“Kuanzia leo lile zoezi letu la kusajili wanachama kama tulivyokuwa tukifanya huko nyuma tumelifunga rasmi na hiyo ni kutokana na kumpata mtu sahihi wa kuturahisishia sisi klabu pamoja na mwanachama mwenyewe, NMB ambayo ukiwa na kadi ya uanachama utaweza kufanya mambo mengi kwa wakati mmoja,” alisema Hersi.
Hersi alisema kwamba moja ya changamoto ambazo zilikuwa zinawaumiza kichwa ni mwanachama au shabiki kulipia ada yake na kutopata kadi yake kwa wakati lakini baada ya muunganiko huo, changamoto hizo wamezipatia suluhisho ambalo anaamini litamfurahisha kila mmoja wao.
Katika makubaliano hayo, Yanga inanufaika katika mradi wa kuongeza idadi ya mashabiki ikiwa ni kwa muda mfupi, pia kukusanya mapato kupitia malipo ya wanachama sehemu zote za Tanzania hata ambako awali hawakufanikiwa kupafikia.
“Wanachama wote ambao wameshajisajili kwenye mfumo, huduma ya kwanza ambayo itapatikana NMB ni kuhuisha uanachama, takwimu ambazo tupo nazo ‘tumesha-shea’ na wenzetu, huduma ya pili, mtu ambaye si mwanachama wa Yanga anaweza kwenda tawi lolote la karibu kwa ajili ya kujiunga na uanachama kwa kupata kadi ambayo itamsaidia kwa matumizi mengine na itakuwa na muonekano wa uanachama wa Yanga,” alisema Hersi.
Ofisa Mkuu wa Biashara na Wateja Binafsi (NMB), Filbert Mponzi alisema pamoja na faida nyingi zitakazopatikana katika ushirikiano wao huo na Yanga lakini kitu kikubwa zaidi ni kurahisisha huduma kwa Wananchi.
“Watakuwa wakienda kwenye matawi yetu ni kama wapo nyumbani vile, hii inakuwa si kadi tu ya kujitambulisha lakini pia unaweza kutumia kwa matumizi mengine ndani na nje ya nchi huku ukifurahia kuwa shabiki na mwanachama wa timu yako ya Yanga,” alisema Mponzi.
