Na mwandishi wetu
Klabu ya Yanga imefunguka kuwa Jonas Mkude ni aina ya wachezaji wanaohitajika Yanga na ikimpendeza kocha mpya wa timu hiyo, Miguel Gamondi, msimu ujao kiungo huyo atakuwa Yanga.
Hayo yameelezwa na Ofisa Habari wa Yanga, Ally Kamwe akizungumza habari zilizopo kuhusu vinara hao wa Ligi Kuu NBC kumuwinda mchezaji huyo aliyeachana na Simba hivi karibuni.
“Jonas Mkude ni mchezaji mzuri hakuna ambaye hajui uwezo wake, ni moja ya viungo wazuri wakabaji tulionao nchini, naamini kwa uzoefu alionao anaweza kuwa na mchango wake kwa timu yoyote atakayokwenda, hakuna timu Tanzania inayoweza kubeza uwezo wake,” alisema Kamwe.
“Kwa hiyo kama itakuwa mipango ya Yanga na uongozi kwa kushirikiana na kocha (Gamondi) wakiona inafaa, tutamkaribisha na naamini wanachama watakuwa na furaha kufanya kazi na kuona mtu mwenye uzoefu anaongezeka kwenye timu yetu,” alisema Kamwe.
Alifafanua kuwa uzoefu na umahiri wa wachezaji ndiyo kitu kikubwa wanachokitafuta Yanga kwa sasa kwa ajili ya kuongeza ubora na ushindani kuelekea msimu ujao katika michuano mbalimbali watakayoshiriki ikiwemo Ligi ya Mabingwa Afrika.
Alisema kwa uwezo wa Mkude ni wazi klabu itakayofanikiwa kumnasa itakuwa imenufaika na kitu kikubwa alichonacho mchezaji huyo ambaye jezi yake namba 20 imestaafishwa Simba baada ya kudumu kwa Wekundu hao kwa miaka 13.
Ingawa Mkude mwenyewe hajaeleza atatua wapi lakini Azam na Singida Fountain Gate pia zimekuwa zikitajwa kumuwania kwa ajili ya uzoefu alionao kwenye ligi ya ndani na michuano ya klabu Afrika.
