Na mwandishi wetu
Hatimaye Yanga imetegua kitendawili cha kocha mpya wa timu hiyo baada ya kumtangaza Miguel Angel Gamondi (pichani) kuwa kocha wao mkuu mpya akirithi mikoba ya Nasreddine Nabi.
Uamuzi wa kumtangaza Gamondi ikiwa ni siku chache zimepita tangu kuachana na Nabi ambaye baada ya kumaliza mkataba wake hakuwa tayari kuongeza mkataba mwingine.
Yanga imemtangaza Gamondi leo Jumamosi ilipokuwa ikiendelea na mkutano wake mkuu unaofanyika kwenye Ukumbi wa Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Mwalimu Julius Nyerere (JNICC), Dar es Salaam.
Ofisa Habari wa Yanga, Ally Kamwe wakati akimtambulisha kocha huyo alisema wamemchukua wakifahamu ni kocha atakayewapeleka mbali kwenye michuano ya klabu Afrika kulingana na wasifu alionao na uzoefu wake soka la Afrika akifundisha kwenye timu mbalimbali.
Gamondi raia wa Argentina amewahi kuinoa timu ya taifa ya Burkina Faso, klabu za Esperance ya Tunisia, Asec Mimosas, USM Alger, Mamelodi Sundowns aliyoipa ubingwa wa Ligi Kuu Afrika Kusini msimu wa 2005-06.
Kocha huyo pia amewahi kuinoa klabu ya Wydad Casablanca ya Morocco aliyoipeleka nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika msimu wa 2020-21.
Duru mbalimbali za michezo zinafafanua kuwa kocha huyo anayeelezwa kupata elimu yake ya ukocha nchini Hispania, Ufaransa, England na Afrika ni mpenzi wa mfumo wa 4-2-3-1 akitumia viungo wengi katikati ya uwanja akipendelea zaidi soka la pasi na kuvutia.
Soka Gamondi amrithi Nabi Yanga
Gamondi amrithi Nabi Yanga
Read also
