Paris, Ufaransa
Straika wa PSG, Kylian Mbappé amesema kwamba Rais wa Ufaransa, Emmanuel Macron hana ushawishi wowote katika maamuzi yake kuhusu timu anayotaka kujiunga nayo.
Mbappe alikuwa akijibu swali kuhusu mambo yake ya baadaye na PSG kama ataendelea kuichezea timu hiyo kwa msimu ujao wa 2023-24 au ana mpango wa kuhama.
Mchezaji huyo ambaye ana mwaka mmoja katika mkataba wake, aliuandikia barua uongozi wa PSG akisema hana mpango wa kuongeza mkataba na klabu hiyo lakini alisema hakuwahi kuitaka imruhusu aihame na kujiunga na Real Madrid.
Mwaka 2021 wakati kukiwa na habari za Mbappe kuihama PSG, Rais Macron alimshauri abaki katika klabu hiyo na kuendelea kucheza soka katika Ligi 1 ya Ufaransa ambayo ndiyo ligi kubwa nchini humo.
Vyombo vya habari nchini Ufaransa mapema wiki hii viliripoti kuwa Rais Macron angefanya juhudi kuhakikisha Mbappe anabaki Ufaransa lakini mchezaji huyo alisisitiza msimamo wake wa kuendelea kuichezea PSG msimu ujao.
“Ushawishi upi ambao rais anao? Katika maisha yangu ya soka, wakati huu mwaka 2023, hakuna, anataka mimi nibaki Paris, lengo langu pia ni kubaki Paris, tuko katika msimamo mmoja,” alisema Mbappe alitoa kauli hiyo jana Alhamisi mbele ya waandishi wa habari kabla ya mechi ya Ufaransa na Gibraltar ya kuwania kufuzu Euro 2024 itakayopigwa leo Ijumaa.
“Je nitahama PSG? Nimeshajibu hlo, nimesema kwamba lengo langu ni kubaki PSG, huo ndio uamuzi wangu pekee kwa wakati huu, niko tayari kurudi maandalizi ya msimu mpya yakianza, sidhani kama barua ilimuua mtu yeyote au nilimkashifu mtu,” alisema.
Klabu ya PSG inadaiwa kuwa njia panda kuhusu Mbappe kwa kuwa amebakisha mwaka mmoja katika mkataba wake, inamhitaji lakini inahofu akiendelea kuwa hapo hadi msimu ujao ataondoka bila ya wao kupata chochote.
Hali hiyo ndiyo inayowafanya vigogo wa timu hiyo kuangalia uwezekano wa kumpiga bei ili walau wapate sehemu ya pesa Dola 196.94 milioni walizotumia mwaka 2017 kumsajili mchezaji huyo kutoka Monaco.
Habari za ndani zinadai kwamba PSG wapo tayari kusikiliza ofa yoyote inayoweza kufikia Dola 161 milioni badala ya kumuacha aondoke bila ya wato kupata chochote.
Na ingawa Mbappe mwenyewe ambaye ana umri wa miaka 24 amesema anataka kubaki lakini habari za ndani zinadai kwamba amekuwa akiwaambia wachezaji wenzake kwamba anataka kuondoka.
Kimataifa Rais Macron hanichagulii timu-Mbappe
Rais Macron hanichagulii timu-Mbappe
Read also
