Paris, Ufaransa
Mshambuliaji wa PSG, Kylian Mbappe ameeleza kuchukizwa kwake kwa jinsi aliyekuwa mshambuliaji mwenzake wa timu hiyo, Lionel Messi alivyokuwa akikosewa heshima kwenye Ligi 1 nchini Ufaransa.
Messi alijiunga na PSG mwaka 2021 kwa uhamisho huru akitokea Barcelona lakini licha ya kuiwezesha timu hiyo kubeba taji la Ligi 1 mara mbili, alijikuta akiwa katika wakati mgumu nchini humo.
Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 35 alijikuta akizomewa na mashabiki wa PSG mara kadhaa ikiwamo baada ya timu hiyo kushindwa kutamba na hatimaye kutolewa kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya.
Kitendo hicho cha mashabiki kimeonekana kumkera Mbappe ambaye amesema kwamba mchezaji huyo ambaye tayari amejiunga na klabu ya Miami ya Marekani, alihitaji kuheshimiwa nchini Ufaransa.
“Hapa tunazungumzia nafasi ya mchezaji bora katika historia ya soka, haijawahi kuwa habari nzuri kwa mchezaji wa hadhi ya Messi kuondoka,” alisema Mbappe.
“Mimi binafsi sijaweza kuelewa kwa nini watu wengi wanaona amani kwa sababu anaondoka, hapa tunamzungumzia Messi, alitakiwa kuheshimiwa lakini badala yake hakupata heshima aliyotakiwa kuipata Ufaransa, ni aibu lakini hivyo ndivyo ilivyokuwa, ni lazima atafutwe mbadala wake haraka iwezekanavyo,” alisema Mbappe.
Mbappe pia alisema kwamba hakuwahi kuwataka mabosi PSG wamruhusu ahamie Real Madrid msimu huu wa majira ya kiangazi badala yake angependa kuendelea kucheza soka na klabu hiyo ya jiji la Paris ingawa alikataa kuongeza mkataba na klabu hiyo.
Mkataba wa Mbappe na PSG unafikia ukomo mwaka 2024 na zipo habari kwamba huenda akajiunga na klabu ya Real Madrid ambayo inasaka mbadala wa mshambuliaji wake Karim Benzema aliyetimkia Saudi Arabia katika klabu ya Al-Ittihad.
PSG nayo inadaiwa kuwa tayari kumpiga bei ili kuvuna pesa ndefu wakati huu ikihofia kumuacha aondoke mwaka 2024 akiwa mchezaji huru na wao kutopata chochote.
