Na mwandishi wetu
Kocha Mkuu wa Yanga, Nasreddine Nabi na msaidizi wake Cedric Kaze kesho Alhamisi wanatarajia kukutana na uongozi wa timu hiyo kuendeleza mazungumzo ya kusaini mkataba mpya wa kukinoa kikosi hicho msimu ujao.
Mikataba ya makocha hao na wengine wa benchi la ufundi imemalizika baada ya mchezo wa fainali wa Kombe la FA (ASFC) juzi mkoani Tanga ambapo Yanga ilibeba taji hilo kwa ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Azam FC.
Makamu Rais wa Yanga, Arafat Haji alieleza kuwa dhamira yao kubwa ni kuhakikisha wanawabakisha makocha hao kwa kuwaboreshea maslahi yao ili kuendeleza mafanikio ambayo wameyapata msimu huu.
“Tutakuwa viongozi wa ajabu kama tutawaacha makocha hawa waliotupa mafanikio kuondoka, tumeandaa ofa nono kwa ajili yao ikiwemo kuwapa mikataba mirefu ili tuendeleze mazuri waliyotupa msimu huu,” alisema Arafat.
Kiongozi huyo alieleza kuwa kabla ya msimu kuisha tayari walishaanza kuzungumza na makocha hao kuhusu kuongeza mkataba na mazungumzo yao yalifikia sehemu nzuri hivyo anaamini baada ya kikao cha kesho, mustakabali wa benchi la ufundi utajulikana.
Haji pia alisema kwamba katika kikao hicho wanatarajia kupokea ripoti nzima ya msimu uliopita pamoja na maboresho ya kikosi chao cha msimu unaokuja wa 2023/24.
Alifafanua kuwa dhamira yao ni kuhakikisha wanawabakisha kundini nyota wote pia walioisaidia timu yao kupata mafanikio waliyokuwa nayo na kusajili wachezaji wachache kwa ajili ya kuimarisha sehemu zilizokuwa na udhaifu.
Baadhi ya wachezaji ambao wanatajwa kusajiliwa na Yanga kwenye dirisha kubwa ni mshambuliaji Ranga Chivaviro kutoka Marumo Gallants ya Afrika Kusini na winga wa TP Mazembe ya DR Congo, Philipe Kinzumbi.
