Na mwandishi wetu
Bondia Seleman Kidunda amewaomba mashabiki wake kujitokeza kwa wingi Juni 30, mwaka huu kwenye Ukumbi wa Mlimani City, Dar es Salaam ili kushuhudia atakavyomchakaza mpinzani wake, Eric Mukadi kutoka DR Congo.
Kidunda ametoa kauli hiyo kuelekea pambano hilo lililopewa jina la Hata Usipolala Patakucha lililoandaliwa na Kampuni ya PAF Limited huku kukiwa na mapambano mengine ya utangulizi zaidi ya manane.
Kidunda alisema kwa upande wake amekuwa akiendelea na maandalizi ya kujiandaa na pambano hilo huku akikataa kuongelea ujumbe wa maneno aliyotumiwa na mpinzani wake kwa kuwa mikakati yake ni kuona anamchapa vibaya katika pambano hilo.
“Nashukuru Mungu naendelea na maandalizi kwa kufanya mazoezi makali kwa sababu najua halitokuwa pambano jepesi kutokana mpinzani mwenyewe, maneno yake hayawezi kunitisha na nisingependa kuongelea alichokisema zaidi ya mimi kujikita kwenye maandalizi kwa sababu atakavyokuja ndivyo tutakavyompokea.
“Ubora wangu unafahamika ninapokuwa ulingoni, sasa kwa nini asipigike kama nafanya mazoezi kwa ajili yake? Lakini ninachotaka kuwaambia kwa sasa mashabiki wangu waje kwa wingi Mlimani City hiyo Juni 30, nataka waje waangalie burudani ya ngumi na siyo maneno kama anavyosema mpinzani wangu,” alisema Kidunda.
Mbali na mapambano mengine ya awali lakini pia bondia Mfaume Mfaume ‘Mapafu ya Mbwa’ naye siku hiyo atazichapa na Nkululeko Mhlongo, bondia kutoka nchini Afrika Kusini.
