Paris, Ufaransa
Klabu ya PSG ya Ufaransa inajiandaa kumpiga bei mshambuliaji wake, Kylian Mbappe katika kipindi hiki cha majira ya kiangazi baada ya mchezaji huyo kusema kwamba hatoongeza mkataba na timu hiyo.
Mkataba wa Mbappe na PSG unafikia ukomo mwishoni mwa msimu ujao ingawa katika mkataba huo kuna kipengele kinachompa nafasi ya kuongeza mwaka mwingine mmoja.
Awali kulikuwapo habari kwamba Mbappe angeongeza mkataba wake na timu hiyo hadi mwaka 2025 lakini baada ya mazungumzo ya miezi kadhaa, hatimaye amesema kwamba hatoongeza mkataba.
Kwa hali hiyo, Mbappe, mshambuliaji nyota wa PSG na timu ya Taifa ya Ufaransa atakuwa huru kuondoka baada ya msimu ujao mazingira yanayoibua mjadala baina ya Mbappe na PSG ambao kwa sasa wanaelekea kubadili sera yao katika kununua wachezaji.
Mabosi PSG inadaiwa wameamua kutokuwa tayari kuona Mbappe akiondoka bila ya wao kupata chochote na ndio maana suala zima la kumpiga bei linapewa nafasi kubwa kwa wakati huu uamuzi ambao utaziweka macho klabu kadhaa kubwa Ulaya zinazomtaka mchezaji huyo.
Real Madrid inafahamika kuwa klabu ya kwanza Ulaya inayoongoza katika kumtaka Mbappe na mwaka jana mchezaji huyo alikataa ofa ya kujiunga na timu hiyo ya Hispania na kuamua kubaki PSG.
Baada ya Karim Benzema kutimkia Saudi Arabia, Real inahitaji mshambuliaji wa kuziba pengo hilo na ingawa hivi karibuni imedaiwa kumtaka Harry Kane wa Tottenham, hiyo haina maana kwamba ikitokea fursa ya kumpata Mbappe klabu hiyo itajiweka kando.
Kimataifa PSG kumpiga bei Mbappe
PSG kumpiga bei Mbappe
Read also
