Barcelona, Hispania
Beki wa zamani wa Barca, Dani Alves anaendelea kusota rumande baada ya kunyimwa dhamana kwa mara ya tatu wakati upelelezi wa kesi ya kubaka mwanamke ukiendelea kwa mwezi wa sita sasa.
Alves aliyewahi kubeba mataji ya Ligi ya Mabingwa Ulaya mara tatu akiwa na Barca, alinyimwa dhamana mara ya kwanza mwezi Februari, akanyimwa mwezi Mei na sasa amenyimwa kwa mara ya tatu jana Jumatatu.
Uamuzi wa kumnyima Alves, 40, dhamana ulifikiwa na mahakama moja ya mjini Barcelona kwa madai kwamba iwapo mchezaji huyo atapewa dhamana anaweza kutoroka.
Juhudi za wakili wa Alves kutaka apewe dhamana ziligonga mwamba licha ya kudai kuwa mteja wake atakuwa tayari kwa masharti yote ya mahakama ikiwamo kushikiliwa hati yake ya kusafiria pamoja na kufuatiliwa kila aendapo kwa kutumia kifaa maalum.
Alves alikamatwa mara ya kwanza Januari mwaka huu akituhumiwa kumdhalilisha na kumbaka mwanamke mmoja katika klabu moja ya usiku mjini Barcelona, tukio analodaiwa kulifanya Desemba 30, 2022.
Mchezaji huyo ambaye pia amewahi kutamba na timu ya Taifa ya Brazil na klabu kadhaa barani Ulaya, amekana kufanya kosa la kubaka badala yake amesisitiza kuwa alichokifanya ilikuwa ni kwa makubaliano.
Ushahidi wa awali kupitia vipimo vya kisayansi umeonesha kuwapo ‘muingiliano’ kutoka kwa Alves kwenda kwa mwanamke anayedaiwa kudhalilishwa.
Kwa mujibu wa sheria ya Hispania iliyopitishwa miaka ya karibuni, kosa la kubaka na yanayohusiana na hayo adhabu ya juu zaidi ni kufungwa jela miaka 15.
Klabu aliyokuwa akiichezea Alves ya Pumas ya nchini Mexico ilifuta mkataba wake na mchezaji huyo mapema mwezi Januari mara baada ya kukamatwa kwa tuhuma zinazomkabili.
Mahusiano Dani Alves aendelea kusota rumande
Dani Alves aendelea kusota rumande
Read also
