Milan, Italia
Mmiliki wa zamani wa klabu ya AC Milan ambaye pia amewahi kuwa Waziri Mkuu wa Italia, Silvio Berlusconi amefariki dunia leo Jumatatu akiwa na miaka 86 na tayari klabu hiyo imetuma salamu za rambirambi.
Katika salamu za rambirambi, taarifa ya AC Milan imeeleza kushtushwa na kifo hicho cha mtu ambaye wamemtaja kuwa hatosahaulika na klabu hiyo na kuungana na wanafamilia, marafiki na washirika katika kuomboleza msiba huo mkubwa.
Kwa upande wake Rais wa Fifa, Gianni Infantino katika salamu zake za rambirambi amemtaja Berlusconi kuwa ni mtu aliyekuwa na maono.
Berlusconi (pichani) mmoja wa mabilionea wa Italia amefariki baada ya kusumbuliwa na maradhi ya saratani ya damu, hali yake ilikuwa mbaya kuanzia Ijumaa na kuwahishwa hospitali kabla ya kufariki dunia leo.
Wakati akiwa mmiliki wa AC Milan, Berlusconi anakumbukwa kwa kufanya mapinduzi makubwa na kuifanya moja ya klabu zenye mafanikio makubwa Italia na barani Ulaya akishinda jumla ya mataji 29.
Berlusconi aliinunua AC Milan klabu ya mji wa nyumbani kwake, mwaka 1986 kabla ya kuiuza mwaka 2017 kwa wawekezaji kutoka China kwa Pauni 628 milioni.
Miongoni mwa mataji makubwa ambayo klabu hiyo iliyapata ikiwa chini ya Berlusconi ni pamoja na mataji matano ya Ulaya na manane ya ligi ya Serie A ambayo ndio ligi kubwa nchini Italia.
Miezi 18 baada ya kuiuza AC Milan, Berlusconi alirudi kwa mara nyingine kwenye soka kupitia kampuni yake ya Fininvest aliponunua asilimia 100 ya hisa za klabu ya daraja la tatu ya Monza.

Kocha wa Real Madrid, Carlo Ancelotti ambaye aliwahi kuichezea Milan ikiwa chini ya Berlusconi mwaka 1988 kabla ya kuwa kocha wa timu hiyo mwaka 2001 na 2009 naye amemkumbuka kiongozi huyo kwa mafanikio yake katika soka.
Ancelloti anakumbukwa kwa kuingia katika mzozo na Berlusconi katika siku zake za mwanzo akiwa kocha baada ya Berlusconi kumlaumu akidai hafurahishwi na uchezaji wa Milan wa kutumia mbinu za kujihami zaidi.
Kocha huyo hata hivyo aliiwezesha Milan kubeba taji la Ligi ya Mabingwa Ulaya mara mbili, na taji la Serie A akiweka rekodi ya kumaliza msimu na pointi 82 katika mechi 34.
Akimzungumzia Berlusconi, Ancelotti alisema kupitia akauni yake ya Twitter: “Huzuni tuliokuwa nao leo haufuti matukio ya furaha tuliyofurahia pamoja.”
