Istanbul, Uturuki
Baada ya kushinda taji la Ligi ya Mabingwa Ulaya na hatimaye kukamilisha msimu na mataji matatu, kocha wa Man City, Pep Guardiola amesema mafanikio hayo yaliandikwa mbinguni kwenye nyota.
Man City jana Jumamosi iliichapa Inter Milan bao 1-0 na kubeba kwa mara ya kwanza taji la Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu huu wa 2022-23 ikiwa tayari imebeba taji la Ligi Kuu England (EPL) na la FA.
“Nimechoka, niko katika utulivu na nimeridhika, ni vigumu kupata ushindi, iliandikwa kwenye nyota (mbinguni), ilikuwa mali yetu,” alisema Pep ambaye pia aliwahi kubeba mataji matatu msimu mmoja wakati akiwa kocha Barcelona.
“Inavutia, ndoto imetimia, watu wote unaowaona hapa walikuwa wakisubiri sijui kwa miaka mingapi, sasa ni haki yao, ni haki yetu, ningependa kumshukuru kila mmoja, haikuwa rahisi kwa timu tuliyokutana nayo, kwa namna wanavyokaba na kufanya mashambulizi ya kushtukiza,” alisema Pep.
“Tulijitoa kwa kila kitu, fainali ndio kama hizi, huwezi kutarajia kucheza unavyocheza kila wakati, tulipambana kama wanyama, ni ndoto, tukio kama hili halitojirudia tena,” alisema Pep.
Hii ni mara ya pili kwa Man City kufikia hatua ya fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya katika misimu mitatu, mara ya mwisho ilikuwa mwaka 2021 waliposhindwa kutamba mbele ya Chelsea waliobeba taji hilo.
Kwa mafanikio hayo Man City sasa inakuwa timu ya pili katika EPL kushinda mataji matatu katika msimu mmoja, timu ya mwisho kufanya hivyo ilikuwa Man United ambayo ilibeba mataji hayo mwaka 1999 wakati huo ikinolewa na Sir Alex Ferguson.
“Ni heshima kuwa sawa na Sir Alex Ferguson. Nimepata ujumbe wake asubuhi hii, na hiyo pia ni heshima,” alisema Pep.
“Watu wanasema natakiwa kushinda mataji matatu kila msimu, mimi ni kocha mzuri lakini hapana huwa napenda mashindano haya hasa kwa sababu tumeshinda, ni sehemu ya historia na wachezaji watakumbuka kwa maisha yao yote,” alisema Pep.
