Na mwandishi wetu
Klabu ya Singida Big Stars imeeleza kuwa hivi karibuni itaitangaza timu yake ya soka ya wanawake ili kukamilisha vigezo vya kanuni za ushiriki wa michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika msimu ujao.
Ofisa Habari wa Singida BS, Hussein Masanza ameeleza hayo baada ya juzi Shirikisho la Soka Afrika (Caf) kutuma ujumbe wa siku ya mwisho wa kupeleka majina ya timu hizo Juni 30, mwaka huu.
Masanza (pichani) alisema kila kitu kimekamilika na tayari wana timu hiyo na wamepanga kuitangaza hivi karibuni kabla ya siku ya mwisho, hivyo mashabiki wa timu hiyo wasiwe na wasiwasi na ushiriki wa timu yao katika michuano hiyo.
“Tumeona taarifa kutoka Caf kuhusu hivyo vigezo, lakini sisi kama Singida tulifahamu mapema maana ni jambo la kikanuni pia hapa Tanzania, ni sharti la kikanuni kwamba timu iwe na timu ya vijana na timu ya wanawake.
“Tumeshajiandaa na hilo na hivi karibuni tutatambulisha rasmi timu ya wanwake ya Singida kwa hiyo hicho sio kigezo cha kutuzuia tusishiriki kimataifa, mashabiki wasiwe na wasiwasi, tukimaliza mechi yetu ya mwisho na kukimalizika hafla ya tuzo za ligi, tutakuwa kwenye wakati mzuri kulitangaza hilo,” alisema Masanza.
Pamoja na hayo, kumekuwa na taarifa za timu hiyo kuinunua timu ya Singida Warriors itakayoshiriki Ligi Kuu ya Wanawake msimu ujao lakini ofisa huyo hakuwa tayari kuzungumzia suala hilo.
