Na mwandishi wetu
Wachezaji 16 wa timu ya taifa ya Tanzania ya soka la ufukweni wanatarajia kuingia kambini Jumapili ya wiki hii kujiandaa na michuano ya pili ya soka la ufukweni kwa Afrika itakayoanza Juni 23 hadi 30, mwaka huu kwenye Mji wa Hammamt, Tunisia.
Akizungumza leo Jumanne jijini Dar es Salaam, kocha mkuu wa timu hiyo, Boniface Pawasa amesema kutokana na muda kuwa mchache kabla ya kuanza kwa mashindano hayo, baada ya wachezaji kuripoti kambini, wataanza mazoezi ya kimbinu na kiufundi kabla ya kucheza mechi za kirafiki.
“Michuano hii imekuja kwa muda muafaka, matarajio yetu ni kufanya vizuri ikiwemo kubeba ubingwa kulingana na utayari wa kikosi chetu lakini kabla ya kwenda kwenye mashindano, tunatarajia kucheza mechi mbili za kirafiki na timu za kombaini ya hapa nchini na Uganda, mechi zote tutacheza hapa nyumbani,” alisema Pawasa.
Pawasa (pichani) ambaye ni beki wa zamani wa kati wa Taifa Stars na klabu ya Simba alisema Tanzania imepata nafasi ya kushiriki michuano hiyo kutokana na uwiano mzuri wa viwango vya kimataifa vya mchezo huo.
Kwa mujibu wa Pawasa timu hiyo ikifanikiwa kutinga hatua ya fainali watapata nafasi kwenda kucheza michuano ya Kombe la Dunia, Agosti 26 hadi Septemba 4, mwaka huu, nchini Indonesia.
Naye Makamu wa Rais wa Kamati ya Olimpiki Tanzania, Henry Tandau alisema Tanzania ilipata nafasi ya kupeleka timu mbili katika mashindano hayo ambazo ni za mpira wa kikapu na soka la ufukweni.
Tandau alisema kwamba timu ya mchezo wa kikapu haikufikia viwango na nafasi hiyo kuchukuliwa na riadha kwa sababu ya kufikia vigezo vilivyotakiwa katika michuano hiyo.
Aliongeza kuwa kwa Tanzania timu ya soka la ufukweni inashika nafasi ya nane kwenye viwango vya Afrika.
Wachezaji 16 walioitwa kwenye timu hiyo ni makipa Shaban Kado (Ihefu FC), Adam Oseja (huru) na Ally Juma (JKU, Zanzibar), Sadiki Salim (Green Warriors), Mtoro Nassoro (Msasani Mabingwa), Ismail Adam (KMC FC), Suleiman Said (Zimamoto, Zanzibar), Abdulrahim Seif na Yahya Haji (Uhamiaji, Zanzibar).
Wengine ni Juma Sultan na Jaruph Rajabu ambao wote ni wachezaji huru, Goodluck Dickson (Friends Rangers), Stephano Wales (Mburahati), Salum Abdillah (Ilala FC) na Samson Baraka kutoka Tanzania Prisons.
Soka Timu ya Ufukweni kambini Jumapili
Timu ya Ufukweni kambini Jumapili
Read also
