Na Hassan Kingu
Jumapili fulani hivi ya mwisho mwezi Novemba mwaka 1993, jiji la Dar au Tanzania ilitawaliwa na ukimya, Simba ilikuwa imetoka kupoteza mchezo wa fainali ya iliyokuwa michuano ya Kombe la Washindi Afrika
Takriban miaka 30 baadaye, Jumapili hiyo inafanana na Jumapili ya leo Juni 4, 2023, jiji la Dar au Tanzania imejaa utulivu, makeke na matumaini yaliyokuwapo katika kuelekea mechi hizo vyote vimetoweka badala yake imekuwa siku ya kujitetea, kama ilivyokuwa Jumapili ile ya Novemba 1993.
Kinachoonekana Jumapili ya leo kinafanana na mwaka 1993, majigambo na majivuno ya kuelekea mechi hizi za fainali yote yalizimika baada ya matokeo ya mechi yenyewe.
Mwaka 1993 Simba ilipoteza mechi ya fainali ya pili nyumbani Uwanja wa Taifa mbele ya Stella Abidjan ya Ivory Coast na kuwafanya mashabiki wake kuwa kimya. Mwaka 2023, Yanga imekutana na hali kama hiyo, imepoteza mechi ya pili ugenini Algeria mbele ya USM Algers.
Kuelekea mechi zote mbili hizi za mwisho mashabiki wa kila timu walijigamba kwa kauli moja kuu ya kuweka historia mpya kwa kuwa timu ya kwanza Tanzania kubeba taji la michuano ya klabu Afrika lakini baada ya matokeo mabaya hali imebadilika.
Mashabiki wa Yanga wakinangwa na wenzao wa Simba wanawaambia na nyinyi fikeni hatua ya fainali, wanajitoa ufahamu katika majigambo yao ya awali ya kubeba kombe, lakini pia wanasahau au hawajui (kama kweli hawajui) kwamba Simba waliwahi kufika hatua kama hiyo miaka takriban 30 iliyopita.
Simba nao mwaka 1993 baada ya kupoteza taji walijigamba kwa kuwaambia Yanga nao wafike hatua ya fainali kama rahisi, wakasahau ile hadithi ya kubeba kombe na kwa kuwa Yanga nao wamefikia hatua hiyo nidhahiri kwamba sasa mashabiki wa timu hizi hawachekani.
Wote timu zao zimefikia hatua ya fainali ya michuano ya klabu Afrika na wote wamepoteza katika hatua hiyo. Hakuna wa kumcheka mwenzake.
Ni kweli kwamba zipo tofauti katika matukio haya, tofauti ya kwanza ni miaka 30, ni mingi mno, baadhi ya mashabiki wa Simba wa sasa walikuwa hawajazaliwa au walikuwa wachanga Simba ikifikia hatua hiyo.
Tofauti nyingine ni aina ya vikosi na makocha, Simba ilifikia hatua hiyo ikiwa na kocha Abdallah Kibaden na msaidizi wake alikuwa ni Entene Eshete kutoka Ethiopia lakini Yanga imeongozwa katika hatua hiyo na makocha wa kigeni, Nasreddine Nabi kutoka Tunisia na msaidizi wake Cedric Kaze kutoka Burundi.
Vikosi pia vilikuwa na utofauti, Simba iliongozwa na wachezaji wa kikosi cha kwanza wazawa watupu kuanzia kipa hadi namba 11 lakini Yanga kikosi chake kilichocheza mechi ya fainali ya pili, asilimia sitini ni wachezaji wageni.
Hili kila mtu analiangalia kwa namna yake lakini kwangu naliangalia kama hatua moja ya maendeleo katika klabu kwamba uwekezaji umekuwa mkubwa kiasi cha kuweza kusajili wachezaji wa kimataifa kutoka mataifa mbalimbali.
Ukiachana na tofauti hizo na nyinginezo, ipo tofuati ya kishabiki ambayo inazungumzwa hasa na mashabiki wa Yanga kwamba mwaka 1993 Simba ilifikia hatua ya fainali ya mashindano tofauti na yasiyo na hadhi na wengine kufananisha na bonanza.
Ukweli ni kwamba mashindano yote haya yanaratibiwa na kuandaliwa na Shirikisho la Soka Afrika (CAF) tofauti ni aina ya wadhamini na labda mabadiliko ya kimfumo ili kwenda na wakati lakini kimsingi yote yana hadhi ya mashindano makubwa ya klabu barani Afrika.
Kuyakataa mashindano ya mwaka 1993 na kuyaona tofauti na haya ya mwaka 2023 ni sawa na kumkataa bingwa wa kihistoria mwenye mataji mengi kwa kusema kwamba alichukua taji la Ligi Kuu Vodacom, au Safari Lager au wakati ule ilikuwa Ligi Daraja la Kwanza na mengineyo na hivyo kuupunguza ubingwa wake wa kihistoria.

Au miaka kadhaa ijayo Total Energies wakiacha kudhamini michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika na kuja mdhamini mwingine, je tutasema Yanga ilifikia hatua ya fainali kwenye bonanza na si michuano ya klabu yenye hadhi barani Afrika?
Nafikiri badala ya mashabiki kubishana na kujadili tofauti ambazo kimsingi hazipo ni bora wakajadili swali moja la msingi kwamba je tulichokiona kwa Yanga kitakuwa na mwendelezo au itakuwa kama hadithi ya Simba, ilipofika mwaka 1993 ikapotea kwenye ramani ya michuano ya klabu Afrika kabla ya kufurukuta kidogo miaka 10 baadaye yaani mwaka 2003.
Je kutakuwa na mwendelezo au ndio homa za msimu, kwamba Yanga nayo itazama kama ilivyokuwa kwa Simba? Kwangu jibu ni hapana kwa kuwa katika miaka ya karibuni klabu za Tanzania zimepiga hatua katika michuano ya klabu Afrika.
Simba na Yanga zote zimekuwa tishio Afrika na hasa Simba imejitahidi kuonyesha uhai katika soka la Afrika ikifikia hatua ya robo fainali mara kadhaa na hata hivi karibuni imeaga Ligi ya Mabingwa Afrika ikitolewa kwa mikwaju ya penalti.
Sitaki kuamini kwamba aina ya uwekezaji unaofanywa sasa ni kiini macho kwamba hakutakuwa na mwendelezo wa kuhakikisha klabu hizi zinaendelea kuwa tishio barani Afrika.
Matumaini yangu ni kwamba kuna siku au miaka michache ijayo taji la michuano ya klabu Afrika litabebwa na timu ya Tanzania.
