Madrid, Hispania
Sasa ni rasmi straika Karim Benzema anaondoka katika klabu ya Real Madrid baada ya kuichezea kwa miaka 14 na kwenda kuanza maisha mapya katika klabu ya Al-Ittihad ya Saudi Arabia.
Benzema, alijiunga na Real Madrid mwaka 2009 akitokea klabu ya Lyon ya Ufaransa na hadi sasa ana rekodi ya kubeba taji la Ligi ya Mabingwa Ulaya mara tano na La Liga mara nne na timu hiyo.
Straika huyo inaelezwa kuwa amepata ofa nono kutoka Al Ittihad na kituo kimoja cha televisheni cha Saudi Arabia kimeripoti hivi karibuni kuwa atasaini mkataba wa miaka miwili.
Benzema ambaye ana mwaka mmoja katika mkataba wake na Real Madrid, ofa nono ya Saudi Arabia imemshawishi kuondoka na hasa kwa ana umri wa miaka 35 ambao ni umri sahihi kwa mchezaji huyo kwenda kwenye ligi tofauti na kukutana na changamoto tofauti.
Uamuzi huo wa Benzema unapingana na alichokisema kocha wake, Carlo Ancelotti Jumamosi hii kwamba ana imani mchezaji huyo ataendelea kuichezea klabu hiyo msimu ujao.
Taarifa ya Real Madrid iliyopatikana leo Jumapili japo haikufafanua kwa undani lakini imeonesha kila kitu kuhusu kuondoka kwa straika huyo tishio aliyeichezea timu hiyo mechi zaidi ya 647 na kufunga mabao 353 akiwa na rekodi ya kubeba mataji 25 na klabu hiyo.
“Benzema amekuwa mfano mzuri kitabia na kiprofesheno, na amewakilisha vyema maadili ya klabu yetu, ana haki zote za kuamua mambo yake ya baadaye,” ilieleza sehemu ya taarifa ya Real Madrid.
Benzema leo Jumapili anatarajia kuichezea Real Madrid mechi yake ya mwisho ya ligi dhidi ya Athletic Bilbao, mechi ambayo inakamilisha msimu wa La Liga wa 2022-23.
Akiwa Saudi Arabia, Benzema ataungana na nyota mwenzake wa zamani wa Real Madrid, Cristiano Ronaldo ambaye kwa sasa anaichezea klabu ya Al Nassr ya huko.
