Budapest, Hungary
Kocha wa AS Roma, Jose Mourinho ameonekana akimvaa mwamuzi Anthony Taylor kwenye maegesho ya magari baada ya timu yake kushindwa kutamba kwenye fainali ya Europa Ligi jana Jumatano.
Mourinho jana kwa mara ya kwanza alipoteza mechi ya fainali ya michuano ya klabu Ulaya ikiwa ni fainali yake ya saba akiwa ameshinda sita za awali baada ya Roma kushindwa kutamba kwa Sevilla. Katika mechi hiyo iliyopigwa mjini Budapest, timu hizo awali zilitoka sare ya bao 1-1 na katika penalti Roma ililala kwa mabao 4-1 jambo ambalo lilionekana kumvuruga mno Mourinho.
Mechi hiyo iliyoonekana kujaa ubabe wa kila aina, ilimfanya mwamuzi kuchukua uamuzi mgumu kwa kutoa jumla ya kadi za njano 13 ikiwa ni rekodi ya kipekee katika mechi ya Europa Ligi.
Baada ya mechi hiyo, video zilimuonesha Mourinho akiwa kwenye maegesho ya magari na kuanza kumkaripia mwamuzi huyo ambaye pia anachezesha mechi za Ligi Kuu England.
Mourinho alimlaumu mwamuzi huyo kwa kushindwa kuipa Roma penalti kipindi cha pili baada ya tukio la mchezaji kuunawa mpira pamoja na maamuzi mengine ambayo anadhani yalimshinda mwamuzi huyo.
“Mwamuzi alijiona kama yeye ni Mhispaniola, matokeo hayakuwa ya haki na kuna mengi ya kuyafanyia tathmini upya,” alisema Mourinho.

“Hii ni fainali ya Ulaya, na kwa aina hii ya uamuzi ni ngumu kukubali, kama tunazungumzia matukio ya mwamuzi, hayakuwa mawili au matatu, ni mengi ukiacha yale maamuzi makubwa, kwa sisi ambao tumekuwa kwenye soka muda mrefu tumebaini haraka kilichokuwa kikiendelea,” alisema Mourinho.
“(Lorenzo) Pellegrini anaanguka kwenye boksi anapewa kadi ya njano, Ocampos (Lucas) anafanya hivyo hivyo hapewi kadi, hii ni kashfa,” alisema Mourinho.
Mourinho ambaye pia alipewa kadi ya njano katika mechi hiyo huenda akakumbana na adhabu ya kufungiwa na Uefa kwa tukio lake la kupokea medali ya fedha kwa timu yake kushika nafasi ya pili lakini akairusha medali hiyo kwa shabiki mmoja kijana mdogo.
Baadaye kocha huyo wa zamani wa timu za FC Porto, Chelsea, Inter Milan, Real Madrid, Man United na Tottenham, alipoulizwa alisema kwamba yeye huwa anatunza medali za dhahabu tu.
Roma inashika nafasi ya sita katika Serie A na Jumapili itaumana na timu ya Spezia inayohaha kujitoa kwenye janga la kushuka daraja, mechi ambayo Roma inatakiwa kushinda ili kujiweka nafasi ya tano.
Iwapo itafanikiwa kushika nafasi ya tano timu hiyo itashiriki michuano ya Europa Ligi msimu ujao vinginevyo ikiangukia nafasi ya sita itashiriki Europa Conference Ligi, michuano ambayo ilibeba taji lake msimu uliopita.
