Na mwandishi wetu
Hafla ya utoaji wa Tuzo za Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) msimu wa 2022/2023 zinatarajia kufanyika Juni 12, mwaka huu kwenye Kituo cha TFF, Mnyanjani mkoani Tanga.
Kwa mantiki hiyo, tuzo hizo zitatolewa siku ya mchezo wa fainali ya Kombe la FA (ASFC) iliyopangwa kupigwa siku hiyo hiyo kwenye Uwanja wa Mkwakwani, Tanga.
Akizungumza leo Alhamisi na TFF TV, Mkurugenzi wa Mashindano wa TFF, Salum Madadi (pchani) alisema wanaamini watakuwa na sherehe kubwa na nzuri mkoani Tanga baada ya mchezo wa fainali.
“Maandalizi yanakwenda vizuri na kwa wenzetu wa Tanga wakiongozwa na Mkuu wa Mkoa wanaendelea vizuri na tunatarajia kuwa na fainali bora kuliko ile ya Arusha,” alisema Madadi.
Kuhusu sehemu ya kuchezea, Madadi alisema uwanja ni mzuri na unaendelea kuandaliwa hivyo wachezaji watacheza kwenye uwanja mzuri na majukwaa na vyumba vya timu vinaendelea kuboreshwa.
“Uwanja upo tayari kwa asilimia 90 kwa sehemu ya kuchezea na kuhusu ‘VIP lounge’ itafungwa nyuma ya uwanja na itakuwa tayari kabla ya Juni 10 hivyo mashabiki wa mpira tukakutane Tanga,” alisema Madadi.
Alisema wameamua kufanya usiku wa tuzo sambamba na siku ya kumkabidhi bingwa zawadi zake tofauti na walivyokuwa wakifanya baada ya mashindano kumalizika.
Fainali ya Kombe la FA itakuwa baina ya mabingwa watetezi Yanga walioifunga Singida Big Stars kwenye nusu fainali dhidi ya Azam FC walioifunga Simba SC.
