Barcelona, Hispania
Kocha wa Barcelona, Xavi Hernandez amesema kumfananisha yeye na aliyekuwa mchezaji mwenzake na kocha wake wa zamani, Pep Guardiola (pichani) hakumsaidii lolote katika kazi yake ya ukocha.
Kwa mara ya kwanza, Xavi ameiwezesha Barca kutwaa taji la La Liga msimu huu tangu mwaka 2019 alipoanza msimu mzima na timu hiyo akiwa kocha lakini amekuwa akikumbana na shutuma kuhusu aina ya soka la timu hiyo.
Katika msimu huu, Barca ina rekodi ya kushinda mechi 11 kila mechi ikiwa na matokeo ya ushindi wa bao 1-0 lakini kumekuwa na hoja za kutaka timu icheze soka la kuvutia katika kufanya mashambulizi kama ilivyokuwa wakati wa Pep ambaye aliinoa timu hiyo kati ya mwaka 2008 hadi 2012.
“Kwa kumuangalia Pep na kisha kutafuta mfanano uliopo kati yake na mimi, ni kama vile kunishusha mimi,” alisema Xavi akimzungumzia Pep ambaye kwa sasa anainoa Man City.
“Sidhani kama ni ulinganio ulio sahihi, ilinitokea hata mimi wakati nikiwa mchezaji, kila mtu alikuwa na yake,” alisema Xavi.
Awali wakati akishutumiwa kwa timu yake kutocheza soka la kuvutia, Xavi aliwahi kusema kwamba hoja hiyo inaonesha jinsi kazi ya kuinoa Barca ilivyo ngumu kwamba hata unaposhinda watu wanahoji ulivyoshinda na hata kuonekana kama vile umepoteza mechi.
Xavi pia alisema kwamba haoni kama anaungwa mkono kwa ujumla katika klabu hiyo kwa mafanikio ambayo ameyapata lakini haoni kuthaminiwa ndani ya klabu ingawa mpango wa kumuongezea mkataba unadaiwa kufanyiwa kazi na huenda makubaliano yakafikiwa hivi karibuni.
“Ndio tutafikia makubaliano hivi karibuni, najua klabu itafanya juhudi kadri iwezekanavyo na hakutakuwa na tatizo, mwisho wa siku nitaongeza mkataba na hatimaye nitaendelea kuwa hapa kwa miaka mingine mingi,” alisema.
