Na mwandishi wetu
Timu ya Azam imeeleza itautumia mchezo wa ligi dhidi ya Coastal Union, kujipanga kikamilifu kuivaa Yanga kuelekea fainali ya Kombe la FA (ASFC) itakayopigwa Juni 12, mwaka huu Uwanja wa Mkwakwani, Tanga.
Azam itaumana na Coastal Juni 6, mwaka huu ikiwa ugenini Uwanja wa Mkwakwani, uwanja ambao Azam imekuwa ikishindwa kupata ushindi dhidi ya Coastal kwa takribani misimu minne sasa.
Ofisa Habari wa Azam, Hashim Ibwe alisema licha ya kuhitaji ushindi Mkwakwani lakini pia ugumu wa mchezo huo watautumia kama maandalizi ya kucheza na Yanga.
“Mchezo dhidi ya Coastal huwa ni mgumu hasa pale Mkwakwani, safari hii tumedhamiria kwanza kuitumia mechi hiyo kama maandalizi kwa mechi yetu inayokuja ya fainali dhidi ya Yanga.
“Tutajaribu kutafuta ushindi unaoshindikana kupatikana miaka yote, ushindi ambao utatuweka rasmi kwenye nafasi ya tatu kabla ya kumalizana na Polisi Tanzania kwenye mechi ya mwisho. Kuhusu maandalizi tunaendelea vizuri, hakuna majeruhi yeyote, tuko sawa kabisa,” alisema Ibwe.
Mchezo huo unatarajiwa kuwa mgumu zaidi kutokana na hali halisi ya Coastal inayohitaji ushindi kujiondoa kudondokea kucheza mechi za mtoano kuwania kutoshuka daraja na kuikosa Ligi Kuu NBC msimu ujao.
