Na mwandishi wetu
Kocha Mkuu wa Simba, Roberto Oliveira ‘Robertinho’ amesema uteuzi wa Mels Daalder (pichani), utakuwa na msaada mkubwa kwake katika mchakato wa kukisuka upya kikosi chake cha msimu ujao.
Mapema wiki hii uongozi wa miamba hiyo ya soka nchini, ulimtambulisha Mels kama mkuu wa idara ya kusaka vipaji (skauti), ambaye atasaidiana na benchi la ufundi katika usajili wa dirisha kubwa kwa ajili ya msimu ujao.
Robertinho alieleza kuwa elimu na uzoefu alionao Mels katika kutambua vipaji vya wachezaji vitasaidia kupata wachezaji sahihi watakaoisaidia timu hiyo kufikia malengo ambayo wamekusudia kuyafikia kuanzia msimu ujao.
“Ni mtu sahihi kwetu, ujio wake utakuwa na faida nyingi kwa klabu ikiwemo kupata wachezaji wenye ubora stahiki kulingana na ukubwa wa Simba, naupongeza uongozi pamoja na bwana Mohammed Dewji (mwekezaji Simba) kwa hiki, naamini Simba ya msimu ujao itakuwa ya tofauti,” alisema Robertinho.
Kocha huyo alisema kuwa amepanga kukutana na Mels hivi karibuni kumsikiliza kipi alichopanga kuanza nacho na yeye kumpa aina za wachezaji anaowahitaji ili waweze kuanza mchakato huo mara moja sababu wanakabiliwa na michuano ya Super League inayotarajia kuanza Agosti, mwaka huu.
Alisema katika kikosi chake cha msimu ujao amepanga kusajili wachezaji wasiopungua wanane wapya ambapo kati yao watano watakuwa wageni na watatu wazawa, baadhi yao tayari wameanza mazungumzo nao na anafurahi kuona mambo yanakwenda vizuri.
