Na mwandishi wetu
Klabu ya Simba SC imemtangaza Mels Daalder (pchani juu) kuwa Mkuu wa ‘Skauti’ katika benchi la ufundi la timu hiyo lililo chini ya Kocha Mkuu, Roberto Oliveira ‘Robertinho’.
Mels raia wa Uholanzi ametangazwa kupewa wadhifa huo Alhamisi hii zikiwa zimepita siku mbili tangu Meneja Habari na Mawasiliano Simba, Ahmed Ally kutangaza kuwa wako mbioni kukamilisha mchakato wa kumsaka mtaalam wa masuala hayo.
Ujio wa Mels kama ilivyokuwa mapendekezo ya Rais wa Heshima wa Simba, Mohammed Dewji kutamfanya mtaalamu huyo ambaye amewahi kufanya kazi na klabu kubwa Ulaya kushiriki katika mchakato wa usajili wa timu hiyo.
Lengo ni kusajili wachezaji wenye viwango bora vinavyoendana na malengo ya timu hiyo ambayo ni kubeba mataji ya ndani na nje ya Tanzania baada ya kuyakosa kwa misimu miwili mfululizo.
Mels ameshiriki kozi mbalimbali za skauti duniani ikiwa ni pamoja na kozi zilizoendeshwa na skauti wa zamani wa Manchester United, David Hobson.
Mels ambaye amewahi kuishi Tanzania, ni shabiki mkubwa wa Simba pia ni mjuzi wa kufanya upembuzi na kwa mujibu wa Mtendaji Mkuu wa Wekundu hao, Imani Kajula, Mels ana ujuzi na ufahamu mkubwa wa ligi ya Tanzania na Afrika kwa ujumla.
“Tuna furaha kumkaribisha Mels ili kuja kuboresha ufanisi kwenye skauti kwani ni eneo muhimu sana kwenye mafanikio ya klabu yetu, tunaendelea na maboresho muhimu kuelekea msimu mpya wa ligi na mashindano ya kimataifa,” alisema Kajula.
Mels anaongea lugha kadhaa ikiwemo ya kwao Uholanzi pamoja na Kiingereza, Kifaransa na Kiswahili kidogo.
