London, England
Kocha Arne Slot (pichani) amekataa kumrithi Antonio Conte katika klabu ya Tottenhham Hostspur akisema kwamba anataka kubaki katika klabu yake ya sasa ya Feyenoord ya Uholanzi.
Slot aliyejiunga na Feyenoord Desemba 2020 akitokea, AZ Alkmaar, katika siku za karibuni amekuwa akihusishwa na mipango ya kuhamia Spurs baada ya klabu hiyo kuachana na Conte, Machi mwaka huu.
Kocha huyo ambaye ameiwezesha Feyenoord kubeba taji la Ligi Kuu Uholanzi maarufu Eredivisie, jana Jumatano alifanya mazungumzo na mabosi wake, mazungumzo yaliyolenga kumuongezea mkataba.
“Nimekuwa nikisikia uvumi kuhusu upande mwingine kunihitaji, kwanza nashukuru kwa hilo lakini ninachotaka kwa sasa ni kubaki Feyenoord na kuendelea na kazi tuliyoianza mwaka jana,” alisema.
“Sijawahi na hakujawahi kuwa na mazungumzo ya kuhama na kikao cha jana (Jumatano) kilikuwa maalum kwa ajili ya kuongeza mkataba, mazungumzo yote na klabu wakati wote yamehusu jambo hilo, napiga hesabu za msimu ujao na Feyenoord,” alisema Slot.
Mara baada ya Spurs kuachana na Conte, Cristian Stellini alipewa jukumu la kuinoa timu hiyo akiwa kocha wa muda lakini alitimuliwa baada ya mechi nne na nafasi yake kukabidhiwa, Ryan Mason huku uvumi wa kocha ajae ukiendelea na jina la Slot likitajwa mara kwa mara.
Spurs imekuwa na mwenendo mbaya kwenye Ligi Kuu England (EPL) hasa katika mechi za mwisho ikishindwa kupambana katika ‘top four’, kwa sasa inashika nafasi ya nane na Jumapili itacheza mechi yake ya mwisho ya EPL dhidi ya Leeds United.
Makocha wengine ambao wamekuwa wakihusishwa na Spurs ni kocha wa zamani wa Bayern Munich, Julian Nagelsmann, Roberto de Zerbi wa Brighton na Vincent Kompany wa Burnley.
Slot mwenye umri wa miaka 44, Spurs inakuwa klabu ya pili ya EPL kuikataa, awali alihusishwa na mipango ya kuinoa Leeds baada ya kutimuliwa kwa Jesse Marsch lakini aliikataa timu hiyo.
