Na mwandishi wetu
Rais wa Yanga, Hersi Said amesema hawana tatizo na kiungo wao, Feisal Salum ‘Fei Toto’ akifafanua wamekuwa wakitimiza anayoyahitaji kwa kutambua ni miongoni mwa wachezaji bora walionao.
Hersi ameeleza hayo leo Jumatano alipokuwa kwenye kipindi cha Power Breakfast cha redio Clouds ambapo ilifika wakati walikwenda kinyume kwa kumpa pesa ya ada yote ya usajili kiasi cha Shilingi milioni 100 kwa mkupuo mmoja wakati ilipaswa alipwe kwa vipindi vinne.
“Wakati GSM inaingia Yanga, tulimwita Fei tukaona ana maslahi madogo na yalikuwa stahiki kwa wakati ule mwaka 2020 ila tukaboresha, tukampa mkataba mpya akawa anapokea mashara wa Sh milioni 4 kutoka milioni 1.5 na ada ya usajili ya Sh milioni 100.
“Fei alileta ombi kuwa ana jambo anataka kufanya na anahitaji pesa hiyo yote. Tukafanya uungwana kwa kumpa pesa yote badala ya milioni 25 kwa kila mwaka, tazama huu uungwana,” alisema Hersi.
Hersi alimsifu Fei kuwa hajawahi kuwa na utovu wa nidhamu, ni mchezaji mzuri na wangependa kuendelea naye, wanatamani kumwona akifika mbali kisoka na Yanga ni sehemu kubwa ya kulifanikisha hilo akitolea mfano sasa wapo fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika.
Alisisitiza kuwa wapo tayari kumpokea Fei na kama tatizo ni maslahi, wapo tayari kuzunguma naye au kama kuna timu inamuhitaji ifike izungumze na uongozi wa Yanga, wabariki uhamisho huo.
Alisema tangu Fei aibue sekeseke la kuvunja mkataba Desemba, mwaka jana, wamekuwa wakimlipa mshahara wake kama kawaida isipokuwa kuanzia Februari, mwaka huu akaunti ya mchezaji huyo imekuwa na tatizo.
Hersi hata hivyo alisema kwamba tayari wamemwandikia barua wakihitaji akaunti mpya ya kumwekea mishara yake ila Fei amekuwa kimya katika hilo.
Hivi karibuni mwanasheria wa Yanga, Simon Patrick alinukuliwa na GreenSports akisema kwamba klabu hiyo inatambua Fei Toto ni mchezaji wao halali hivyo watampa medali za ubingwa kama wachezaji wengine.
Yanga tayari imeshatangazwa bingwa wa Ligi Kuu NBC msimu huu wa 2022-23 na sasa inapigania makombe mawili ikiwa katika hatua ya fainali ya Kombe la FA (ASFC) pamoja na Kombe la Shirikisho Afrika.
